Na Daniel Mbega, Mwanza
SHAHIDI wa sita katika kesi ya mauaji ya Aaron Nongo mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Mkaguzi wa Polisi (Inspector) David Mhanaya, ameanza kutoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.
Mbele ya Jaji Robert Makaramba anayesikiliza Shauri hilo namba 213 la mwaka 2014, shahidi huyo ametumia siku nzima kutoa ushahidi wake akiongozwa na mawakili wa serikali Emil Kiria, Esther Majaliwa na Robert Kilando.
Hata hivyo, Jaji Makaramba aliahirisha kesi hiyo hadi keshokutwa Mei 14, 2015 baada ya kutokea mgongano wa kisheria katika masuala ya vidhibiti kufuatia pingamizi la Wakili Makwega wa upande wa utetezi, hivyo siku hiyo atatoa uamuzi kuhusiana na pingamizi hilo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Chacha Jeremia, Mathew Jeremia Mlimi, Paschal Lugoye Mashiku na Alex Joseph maarufu kama Bugwema Silola Jangalu.
Marehemu Nongo aliuawa Juni 26, 2009 majira ya saa tatu usiku akiwa nyumbani kwake Ibanda Relini, jijini Mwanza ambapo wauaji hao walimkata usoni na kisha kumkata miguu yake yote miwili na kutoweka nayo pamoja na meno mawili ya mbele.
No comments:
Post a Comment