Ndugu Wananchi,
Magonjwa yaliyokuwa
hayapewi kipaumbele, hususan Kichocho na Minyoo ya tumbo yameathiri sehemu
kubwa ya jamii katika mkoa wetu wa Mwanza. Magonjwa haya huleta mahangaiko
makubwa kwa wananchi hasa kwa watoto ikiwemo
upungufu wa damu, kuzorotesha ukuaji, kupunguza mahudhurio ya watoto shuleni na
pia kutofanya vizuri katika masomo yao .
Ugonjwa wa Kichocho husababisha Saratani
ya Kibofu cha mkojo ambayo haina tiba hadi sasa. Minyoo ya tumbo inaweza kusababisha Utumbo
kuziba na mtu kulazimika kukatwa utumbo, Minyoo ikiingia kwenye ubongo huleta
dalili kama za kifafa vilevile minyoo
huathiri Ini na endapo
muathirika hatawahi kupata matibabu,
dalili zote hizi husababisha Mauti. Magonjwa haya ni moja kati ya vyanzo vikuu
vya umasikini katika familia, jamii, na taifa kwa ujumla.
Aidha, takwimu
zinaonesha kuwa wagonjwa walioathirika kwa saratani ya kibofu cha mkojo na hasa
wakazi wa kanda ya ziwa kwa asilimia kubwa chanzo chake ni maambukizi ya
kichocho.
Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania
iliridhia tamko la Shirika la Afya Duniani linalokusudia kudhibiti au kutokomeza
magonjwa haya ifikapo mwaka 2020, na ili kutekeleza azma hiyo. Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii imetengeneza mpango kazi wa miaka mitano wa Utekelezaji wa shughuli
mbalimbali za udhibiti wa magonjwa haya.
Ndugu Wananchi,
Tafiti
zilizofanyika mwaka 2005 zimeonyesha uwepo wa maambukizi ya ugonjwa wa Kichocho mkoani Mwanza yapo juu kuliko maeneo
mengine nchini. Utafiti huo ulionyesha maambukizi ya Kichocho yapo kati ya
asilimia 12.7 hadi 87.6 nchini.
Utafiti huo unaonesha kwamba ugonjwa wa
kichocho umeenea zaidi maeneo ya kando kando ya ziwa Viktoria na kiwango cha
maambukizo ni zaidi ya 80% na kwa minyoo ya tumbo ni hadi 100%.
Na katika jamii za watoto wenye umri wa
kwenda shule, tafiti kwa njia ya parasitologia, maambukizi ya ugonjwa huu ni
zaidi ya 50%. Kwa kiwango hicho cha maambuzi, kwa mujibu wa tafiti na maelekezo
ya kitaalam ya Shirika la Afya Duniani (WHO), jamii inapaswa ipewe dawa za
kukinga na kutibu.
Tangu mwaka 2009
wizara ilizindua mpango wa udhibiti wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele
katika mikoa ya mitano kwa kuanzia, na hadi mwaka 2012 mpango huu tayari
ulikuwa umetekelezwa katika mikoa 14 na hadi mwishoni mwa mwaka jana (2014) umekuwa
ukitekelezwa katika mikoa 17 ikiwemo
Mwanza iliyoingia katika mpango mwaka 2013.
Hadi sasa, mpango huo unaratibu
shughuli zake katika mikoa 21 ikiwemo Kilimanjaro, Arusha, Simiyu na Geita
iliyoingizwa katika mpango mwaka huu wa 2015. Lengo la mpango kwa sasa ni kuifikia
mikoa ya Shinyanga, Mara na Kagera mapema iwezekanavyo ili kudhibiti magonjwa
haya ifikapo mwaka 2020.
Ndugu Wananchi,
Mkoa unawajulisha
wananchi na wakazi wote wa mkoa wa Mwanza
kuwa tarehe 26 na 27 Mei 2015 tutaendesha kampeni ya ugawaji dawa za kukinga na kutibu magonjwa ya Kichocho
na Minyoo ya Tumbo. Walengwa wa kumeza dawa hizi ni watoto wote wenye umri wa kuanza shule ya msingi
walioandikishwa na wasioandikishwa.
Kampeni hii
itaendeshwa na watalaam wa huduma za afya wakishirikiana na Walimu katika shule
zote za msingi waliopatiwa mafunzo maalumu ya ugawaji wa dawa hizi. Kabla ya
unywaji wa Dawa hizi Mtoto anatakiwa ale chakula na katika muda usiozidi masaa 2 baada ya kula awe amepatiwa dawa
hizi; chakula hicho kitaandaliwa shuleni.
Hivyo kila Mzazi katika mkoa wa Mwanza anaombwa amruhusu mtoto wake aende kumeza dawa hizi muhimu
ili ajikinge na kupata tiba ya magonjwa haya hatari kwani huduma hii ya dawa za kinga tiba inatolewa bila malipo
kwa kila mtoto.
Dawa hizi
zimethibitishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa ni salama, na hazina
madhara yoyote kwa afya ya binadamu zinapomezwa kwa kufuata maelekezo yanayotolewa
na wahudumu wa afya na Walimu waliopatiwa mafunzo.
Dawa zitakazohusika
ni za Praziquantel za kudhibiti Kichocho na Albendazole za kudhibiti Minyoo ya tumbo ambazo zitatolewa kwa watoto
wote wenye umri wa kwenda shule, walioandikishwa na ambao hawakuandikishwa.
Ndugu Wananchi,
Ni matumaini yetu kuwa Wazazi mtawaruhusu watoto wajitokeze kwa
wingi ili kumeza dawa hizi kwa maendeleo ya afya za watoto wetu na Jamii kwa
ujumla. Nawaombeni sana ,
muendeleze sifa nzuri ya Mkoa wetu kwani umekuwa ukifanya vizuri miaka yote
katika suala zima la chanjo.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
IMETOLEWA NA OFISI YA MKUU WA MKOA MWANZA
No comments:
Post a Comment