HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 03, 2015

Nyalandu aahidi kuwapa gari polisi

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiwa ndani ya gari la Polisi wakati wa ziara yake wilayani Biharamulo. (Picha na Loveness Bernard)
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro nyalandu akikagua mitego ya kutegea wanyama iliyokamatwa kutoka kwa majingiri katika mapori ya akiba ya Ibanda na Rumanyika mkoani Kagera, wakati wa ziara yake ya kutembelea mapori hayo.

NA  LOVENESS BERNARD, BIHARAMULO
 
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ameahidi kutoa gari katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kyerwa kutokana na ushirikiano wao waliounyesha kwa askari wa wanyamapori katika kulinda rasilimali za nchi.

Waziri Nyalandu alitoa ahadi hiyo kuona  uchakavu wa gari lililokuwa likitumiwa na askari wa kituo hicho. 

 Gari hilo lilishindwa kupanda mlima wakati walipokuwa wakimsindikiza kutoka Uwanja wa Ndege wa Pori la Akiba la Ibandana Rumanyika.

Katika ziara hiyo, Nyalandu alionyesha ujasiri wa kulikwamua gari hilo la polisi lililokuwa limeshindwa kupanda mlima.

Mbali na kutoa ahadi hiyo aliahidi  kutoa gari lingine kwa Kituo cha Wanyamapori cha Ibanda na Rumanyika ambao pia gari wanalotumia halitoshelezi mahitaji yao kutokana na ukubwa wa pori hilo.

Aidha, Meneja wa Pori la Akiba la Ibanda Rumanyika, Linus Chuwa aliomba Idara ya Wanyamapori nchini kubadilisha matumizi ya mapori hayo kutoka kuwa pori la uwindaji kuwa pori la utalii wa picha.

Hatua hiyo inatokana  na kupungua kwa wageni wanaokwenda kufanya shughuli za uwindaji katika pori hilo ambapo kwa mwaka mzima  2014 walipata wawindaji wawili tu. 

Alisema wawindaji hao walipelekwa Kampuni Said Kawawa Hunting Safaris.

Akizungumzia matatizo yanayolikabili pori hilo alisema kwa hivi karibuni kumejitokeza wimbi la ujangili la kuua tembo na wanyama wengine katika maeneo ya ranchi za Kitengule, Kagoma na Misenyi ambapo jumla ya tembo wanne waliuawa.

Mapori hayo ya akiba ya Ibanda na Rumanyika kuna rasilimali za wanyamapori aina mbalimbali kama chui, tembo, kiboko, ngiri, nyemela, korongo, pofu, swala pala na nyati.

No comments:

Post a Comment

Pages