Na Mwandishi Maalum
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba ameagiza
taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ziendeleze michezo kwa wafanyakazi wao
makazini na kuhakikisha wanashiriki michuano
ya mashirika ya umma na taasisi zenye uwezo kama Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) kushiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.
Dk. Tizeba amesema hayo mwishoni mwa wiki Jijini Mwanza
wakati akiwapongeza wanamichezo wa timu ya Wizara ya Uchukuzi iliyoshiriki michuano
ya michezo ya Mei Mosi na kuibuka washindi wa jumla.
“Mnataka kuniambia Bakhressa (Salim Bakhressa, mmiliki wa
timu soka ya Azam inayoshiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara) ana fedha kuliko
Bandari, “ Waziri Dk. Tizeba aliwauliza wanamichezo hao wakati akitia msisitizo
kwa Mamlaka ya Bandari, shirika kubwa, kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu hiyo
nchini.
Alisema timu za taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi
na hasa zenye uwezo mkubwa wa kifedha kama Bandari zina fursa ya kushiriki hata
Ligi Kuu kama ilivyo Azam ya Bakhressa. Alizitaka zijiandae mapema kwa michezo
ya Mesi mosi kwa kuandaa michuano ya ndani na
ya taasisi ili kupata timu bora ya wizara. Alisema vikombe 12 ni
vichache sana na akataka mwakani viwe zaidi ya 40 kwani uwezo huo wanao.
Aliwaeleza wanamichezo hao waliotwaa vikombe 12, vitano vya
ushindi wa kwanza kuwa, michezo ni sehemu ya kazi na hivyo kumwagiza Mkurugenzi
wa Raslimali Watu na Utawala(DAP) wa Wizara ya Uchukuzi, Immaculate Ngwalle
kuwaagiza watendaji wa taasisi za wizara hiyo kuipa michezo umuhimu.
Alisema ni aibu kwa taasisi nane tu kati ya 15 za Wizara
hiyo kushiriki Mei mosi kwa madai ya ukata na kuwataka watendaji wa taasisi
hizo kuhakikisha wanaweka bajeti ya michezo kwenye bajeti yao kuu vingnevo,
hataipitisha kwani wafanyakazi wanapaswa kushiriki michezo kama sehemu ya kazi
zao pia.
Aliwataka watendaji wa taasisi ambazo zimeajiri wafanyakazi
wa muda kwa muda mrefu ambao ajira zao si za kudumu kuomba kibali cha ikama iii
wathibitishwe kazini ili washiriki michezo hiyo bila utata kwani ni haki yao na
huchangia ushindi kama walivyofanya kina mama wa Bandari walioshinda mchezo wa
kuvuta kamba ingawa ni vibarua. Alihoji kama taasisi hizo haziwahitaji, vipi
ziendelee nao muda mrefu.
Wanamichezo 100 wa
timu ya Uchukuzi walioshiriki walitoka Bandari (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Mamlaka ya Hali ya Hewa
(TMA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga(TCAA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),
Chuo cha Masuala ya Bahari (DMI) na Wizarani. TAA iliongoza kwa kutoa
wanamichezo 56 ikifuatiwa na Bandari 26 na ya mwsho ni NIT (1).
Michezo waliyoshiriki ni soka walioyoibuka washindi wa tatu,
baiskeli, netiboli, bao, kuvuta kamba, karata. Mbali ya Waziri, DAP, Mama
Ngwalle aliwapongeza kwa ushindi huo mnono na kuwataka waongeze bidiii zaidi
mwakani. Manahodha wa timu zilizoshinda walimkabidhi Dk. Tizeba vikombe vyao.
IMETOLEWA NA GODFREY LUTEGO, AFISA UHUSIANO, MAMLAKA YA
VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA
No comments:
Post a Comment