Walalahoi na Wadau; Bajeti inatuumiza na ina maneno matupu..!!
Na Bryceson Mathias, Mvomero, Morogoro.
ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekosti na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii nchini, William Mwamalanga, amesema, Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016 iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, ni bajeti iliyomshangaza, maana haisemi ukweli.
Wakati huo huo, wasomi, wananchi wenye kipato kidogo, wakulima, wafugaji na wafanyabiashara, wamesema Bajeti hiyo ni ya kuendelea kuwaumiza na yenye maneno matupu, huku wakidai, wao wanaendelea kufanywa manamba wa kuwazalishia wachache wanaonufaika nayo.
Wakihojiwa kwa nyakati tofauti, kwa upande wake Askofu Mwamalanga alisema, hii ni Bajeti sindikizi, na kwamba alidhani itakuwa ya kimkakati, lakini unapopandisha mafuta hata ya taa kwa wanyonge, basi jamii inajifunza kuwa watawala hawajaichukia dhambi ya umaskini, na kwa maana hiyo utawala umefitinika kama Babeli.
“Naishangaa Bajeti iliyosomwa, kwa sababu si ya ukweli ni ya uongo, maana inakadiria kitu ambacho hakipo, ambapo hata msomaji akisingizia, haiendi sambamba, ni sawa na mtu anayesema sina dhambi wakati anajidanganya mwenyewe.
“Mwaka 2000, Marekani walitaka Soko Huru kwa nchi za Afrika (AGOA) ziuze bidhaa za kilimo kwao; wakati nchi yetu ikiuza asilimia 3%, Kenya ilikuwa inauza bidhaa asilimia 18%, na hadi leo, sisi tukiwa hatuendi popote, Kenya inauza asilimia 98%”.. aling’aka Askofu Mwamalanga.
Msomi wa Tasnia ya Habari Morogoro, Thadei Hafigwa, alisema, baadhi ya viwanda vidogovidogo, mitambo na magari, vinatumia mafuta, hivyo nyongeza ya bei kwa mafuta ya taa, petrol na dizeli, ni mzigo kwa wananchi, hivyo Serikali iwe na ubunifu wa vyanzo vingine vya mapato.
“Ni Bajeti isiyotekelezeka maana haiendani na uhalisia, 2014/2015 wizara zimetekeleza kwa asilimia 40%, kwa mtindo huo mwananchi ataendelea kupigika kutokana na kupanda kwa nishati ya mafuta, ambayo eti fedha zake zinakwenda REA jambo linaloonekana ni la kusadikika,” alisema msomi, Elizeus Rwegasira wa Morogoro.
Aidha, mkulima wa Lungo Mvomero, Abeid Msangi, alisema, Bajeti hiyo imekiuka sera ya kukasimu rasilimali (Decentralization of Resources) na badala yake, inataka imiliki rasilimali (Centralization of Resources) yenyewe na kuzigawa, ambapo itabaki na asilimia 70% na kugawa kwa walalahoi asilimia 30%, jambo linalowaumiza.
No comments:
Post a Comment