HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 28, 2015

Wakulima waruhusu maiti waliyoizuia ichukuliwe na Polisi

 Na Bryceson Mathias, Kilosa

HATIMAYE wakulima wenye hasira wa Kijiji cha Mbigiri, Kilosa Morogoro, wameruhusu maiti ya Maiko Ngorongoro(40), aliyeuawa na vijana zaidi ya 40 wa jamii ya Kimasai (morani) kwenye mashamba ya wakulima, ichukuliwe na polisi, baada ya jana kumzuia asichukuliwe hadi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajabu Rutengwe, afike.

Tukio la mauaji ya Ngorongoro yalitokea huku kukiwa na sintofahamu ya viongozi wa kijiji hicho, Hamad Ibrahim (Mwenyekiti), Jacob Mvungi (Mtendaji wa Kijiji) na Maftaha Hamis (Mwenyekiti wa Tawi la Chadema-Mbigiri), wakiwa bado wako mahabusu Kilosa, wakitakiwa kueleza ni nani waliosababisha kuuawa kwa ng’ombe takriban 300 kwa kukatwa miguu na majereha mengine, Machi mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tuwatugawe, Daniel Shabani, alsema wakulima wameiruhusu maiti hiyo ichukuliwe na polisi, baada ya kuwa na maridhiano baina ya uongozi wa Wilaya ya Kilosa na mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro aliyemwakilisha, Dk. Rutengwe.

Hata hivyo wakati wakulima hao wakiridhia maiti hiyo kuchukuliwa na Polisi baada ya maridhiano na uongozi wa serikali ya Wilaya ya Kilosa na Mkoa wa Morogoro, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha wafugaji cha Mabwegere, Mika Kashu, amekamatwa na polisi kufuatia tukio hilo.

 Kukamatwa kwake kunatokana na vijana zaidi ya 40 (Morani) wa kifugaji, ambao jana waliwashambulia wakulima waliokuwa mashambani wakilima na wakamuua, Ngorogoro, kwa kumchoma mikuki ubavuni na kumpasua kichwa.


 Toka jana baada ya mauaji hayo, wakulima walisikika wakiilalamikia Serikali Kuu kwamba, vyombo vyake vya usalama wilayani Kilosa na mkoani Morogoro, vimekuwa vikiwapendelea na kuwabeba wafugaji kila yanapotokea majanga baina yao, wakidai kuna kiashiria cha rushwa kinawabeba.

“Wafugaji wakipata janga, japo ng'ombe mmoja kukamatwa anapokula mazao yetu, viongozi wa serikali, polisi ya wilaya na mkoa, wanahamia eneo la tukio haraka wakiwa na magari, silaha na kila kifaa cha ulinzi, lakini mkulima akifa, polisi wanakuja kwa kusuasua,” alisema Shabani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alipopigiwa simu jana kwenye simu yake ya kiganjani atoe ufafanuzi, simu yake ilipokewa na mlinzi wake, na alipoelezwa juu ya tukio hilo alisema sawa bila kutoa ushirikiano.

No comments:

Post a Comment

Pages