Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Pratap Ghose (katikati) akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi kuhusu ushirikiano wao na chama cha Maalbino Tanzania. Kulia ni Mkurugenzi wa Masoko wa Zantel, Progress Chisenga, na Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Tanzania, Ernest Kimaya.
Mkurugenzi wa Masoko wa Zantel, Progress Chisenga (kulia), akizungumza katika mkutano huo.Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Tanzania, Ernest Kimaya (katikati), akizungumza katika mkutano huo wakati akiishukuru Zantel kwa msaada huo kwa chama hicho.
Meneja wa Chapa ya Zantel, Arnold Madale (kulia), akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu msaada huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Pratap Ghose(wa nne kulia), akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni tano kwa Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Tanzania, Ernest Kimaya (kushoto) kwa ajili kusaidia chama cha Maalbino Tanzania kutoa elimu kwa umma kuhusu changamoto walizonazo. Wengine ni maofisa kutoka chama cha Maalbino na maofisa wa Zantel.
Na Dotto Mwaibale
Kampuni ya simu za mikononi ya Zantel
leo imekisaidia Chama cha Maalbino Tanzania katika mpango wake wa kusambaza
elimu juu ya ulemavu wa ngozi kwa jamii pamoja na msaada wa jumla ya shilingi
milioni 5 ambao unalenga kusaidia uendeshaji wa shughuli zake hapa nchini.
Zantel kwa kushirikiana na Chama Cha
Maalbino kitajikita kutoa elimu hii kwa kusambaza ujumbe mfupi kwa wateja wake
pamoja na kutumia vipindi vyake inavyodhamini ili kupeleka ujumbe kwa jamii
kiujumla.
Pamoja na hiyo pia, Zantel inajipanga kutumia mikutano ya wafanyakazi pamoja na
matamasha ili kuhakikisha ujumbe kuhusu ulemavu wa ngozi unawafikia watu wengi
zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi,
Mkurugenzi Mtendaji wa Zantel, Pratap Ghose alisema mchango huo katika
kuwawezesha Chama cha Maalbino ni sehemu ya huduma za kampuni yake kwa jamii.
“Tatizo kubwa ni ukosefu wa elimu
miongoni mwa wanajamii, na kwa hakika hatua kubwa imepigwa katika kupambana na
tatizo hili tayari, na sisi kama Zantel tunaamini kwa kutumia uwezo wetu kama
kampuni ya simu tunaweza kushiriki kulimaliza tatizo hili la mauaji ya ndugu
zetu’ alisema Pratap.
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012,
Tanzania ina jumla ya watu wenye ulemavu wa ngozi 5,200 na wengi wao wanaishi
kanda ya ziwa, na toka mwaka 2009 jumla ya kesi 155 zinazohusu walemavu wa
ngozi zimeripotiwa kwa vyombo vya sheria kwa mujibu wa taasisi ya Under the
Same Sun.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama
cha Maalbino Tanzania, Ernest Kimaya, ameipongeza kampuni ya Zantel kwa mchango
wao akisema utasaidia sana katika juhudi zao za kupigania haki za walemavu wa
ngozi nchini.
‘Watu wenye ulemavu wa ngozi ni kama
binadamu wengine wa kawaida, hivyo tunaiomba jamii isiwatenge ndugu zetu hawa’
alisema Kimaya.
Bwana Kimaya pia aliomba
wadau wengine wajitokeze kuwawezesha walemavu wa ngozi waweze kukabiliana na
changamoto wanazokumbana nazo.
“Jamii yetu ya walemavu
wa ngozi ina matatizo mbalimbali, hivyo tunazidi kuwaomba watu binafsi,
serikali pamoja na makampuni mbalimbali wazidi kujitokeza kusaidia kundi hili
la jamii’ alisisitiza Kimaya.
No comments:
Post a Comment