*Mtanzania wa kwanza
kufanya biashara ya korosho nchini Vietnam
Mfanyabiashara
wa kimataifa anayejihusisha na biashara
ya mazao, Abbas Maziku akifafanua jambo
katika mahojiano na Tanzania Daima kuielezea shauku yake ya kutaka kuwa
mfanyabiashara mkubwa kama Mohammed Dewji(Mo).
Mfanyabiashara wa kimataifa, Abbas Maziku akiwa
ofisini kwake maeneo ya Posta Mpya
jijini Dar es Salaam.
Mfanyabiashara wa kimataifa, Abbas Maziku akiwa na mfanyabiashara tajiri na mwenye umri mdogo
anayemiliki Kampuni ya Mohammed Interprises(MeTl)Mo Dewji.
Magunia
ya korosho yakisubiri kupakiwa kwenye makontena
tayari kwa kusafirishwa kwenda nchini Vietnam
ambapo mfanyabiashara, Abbas Maziku hufanya nao biashara kwa mkataba maalumu.
NA MWANDISHI WETU
BIASHARA ya
kusafirisha mazao ina ushindani mkubwa kutokana na kutawaliwa na matajiri
wenye asili ya Kiasia.
Sababu hiyo
imewafanya Waafrika wengi kutokuwa na uthubutu katika biashara hiyo kwa
kuhofia kutofanikiwa na kujitanua kibiashara.
Mbali na
ugumu huo lakini pia wengi hasa Watanzania wamejikuta wakiishia kuwa
wafanyabiashara wa kawaida na kupoteza fursa za kimataifa.
Kupoteza
fursa muhimu za kimataifa kumefanya wakose nafasi ambazo zingeweza kuwafanya kufikiri
nje ya boksi.
Makala hii inamwangazia
mfanyabiashara wa kwanza wa Kitanzania kufanya biashara ya kusafirisha korosho
kwenda nchini Vietnam,
Abbas Maziku.
Alipoanzia
Maziku anasema
alianza biashara ya kusafirisha mazao mnamo mwaka 2013 baada ya kuvutiwa na
mjomba yake ambaye alikuwa na mashamba yaliyokuwa na mazao mbalimbali.
Miongoni
mwa mazao ambayo Maziku alianza nayo na anaendelea nayo ni korosho, ufuta,
mbaazi, choroko, mtama, alizeti, mashudu ya pamba na pilipili Manga.
Anasema
mazao hayo huyakusanya kutoka kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, wakulima
pamoja na kwenye minada inayofanywa na vyama vya ushirika katika
mikoa ya Lindi, Mtwara, Dodoma,
Singida, Shinyanga na Tanga.
Anayasafirisha
kwa njia gani?
Akizungumzia
jinsi anavyosafirisha mazao hayo, Maziku anasema hutumia gari kuyatoa mikoani
hadi kuyafikisha maghalani na kuyahifadhi kabla ya kufungasha.
“Wakati wa
kuyafungasha unapofika huwa nayafungasha kwa kutumia vibarua na katika
vifungashio vyangu huwa na nembo inayoonyesha jina la kampuni yangu
na baada ya hapo sampuli hupelekwa katika maabara za kupima ubora wa mazao
kimataifa iitwayo SGS na ndipo hufuatiwa na hatua ya mwisho ya
usafirishaji ambayo huwa natumia meli za mashirika mbalimbali ikiwamo
IPTL, MAERSK na nyinginezo kwa ajili ya kwenda nchini Vietnam,”
anasema Maziku.
Anabainisha
baada ya hatua zote hizo hufuata taratibu zinazotakiwa ikiwemo kulipia ushuru
kwa Mamlaka ya mapato nchini, (TRA), wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na
ufugaji, wanasheria pamoja na maofisa wa Usalama wa Taifa ambao huhakikisha
hatua zote halali zimefuatwa.
Maziku
anasema kwamba kwa biashara za kimataifa Shirika la Viwango (TBS)
na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hawahusiki bali wahusika wakuu ni SGS.
Anajiendeshaje
kibiashara?
Maziku
anajinasibu kwamba biashara ya kuuza mazao nje ya nchi ina ushindani
mkubwa.
Anasema anakumbuka
alianza na mtaji wa sh. 2,000,000 na sasa anazungumzia mtaji wa sh. milioni 200.
“Si
rahisi kufika nilipofikia kwasababu biashara hii ina ushindani
mkubwa, ninashindani na matajiri wakubwa wenye uwezo wa kujipangia bei za mazao
hivyo ingawa nimepiga hatua lakini bado ninahitaji kupanua biashara yangu
zaidi na zaidi”anasisitiza.
Anaeleza
kwamba mwaka 2013 alipata hasara ya baada ya ubora wa mazao aliyopeleka kupimwa
na kuonekana upo kwenye kiwango cha 48 badala ya 51 inayotakiwa hivyo ilimpa
wakati mgumu na kuyumba kibiashara na mtaji wake kukata ndipo
alipolazimika kukopa fedha benki ambapo hadi sasa bado analipa deni hilo.
“Nilipata
hasara kubwa sana ambayo hadi leo hii bado
ninalipa hilo
deni nililokopa benki ingawa pia fedha kutoka kwenye vyanzo
mbalimbali vya mapato ya biashara zingine ninazozifanya zinaendelea kuifanya bishahara
ya mazao kwenda nje ya nchi iendelee kuwepo,” anasema.
Vikwazo vya
kibiashara
Maziku
anakwenda mbali na kueleza katika jambo lolote lenye mafanikio vikwazo huwa
havikosekani lakini kubwa katika ni mtaji.
Pia analia
na ukiritimba unaofanywa na benki mbalimbali ambao hutaka dhamana
kubwa kuliko uwezo wa mfanyabiashara.
Ukiachilia
mbali suala la benki, Maziku anasema kikwazo kingine ni ukiritimba kwenye
vyama vya ushirika katika suala zima la upangaji wa bei ambazo hukinzana
na bei ya katika soko la dunia hivyo inakuwa ngumu kwa wafanyabiasahara kufikia
malengo kutokana na kuepuka kupata hasara.
Aidha,
anataja vikwazo vingine ni wizi wa fedha unaofanywa na baadhi ya watu anaowaamini
kumnunulia mazao ambao hutoroka na
fedha hivyo kufanya suala la uaminifu kuwa mdogo na vikwazo vya ubora wa
mazao.
Mafanikio
Akizungumzia
mafanikio Maziku anabainisha, tangu alipoanza biashara ameweza kuwa na
kampuni mbili zijulikazo kama Agromart Company
Limited (GEFU) na Lyone Investment Company Limited ambazo kwa pamoja
ameajiri wafanyakazi watano akiwemo Ofisa Rasilimali Watu, Mhasibu, katibu
Muhtasi, Mwanasheria na Meneja Mwendeshaji wa shughuli za kampuni.
Anaeleza
kwa biashara anayoifanya ameweza kujenga nyumba yake mwenyewe, kumiliki usafiri
na kupata fursa za kusafiri nchi mbalimbali kuhudhuria makongamano na
maonyesho ya biashara ya mazao jambo ambalo limemkutanisha na watu na kupanua
wigo wa biashara yake kimataifa.
Maziku anasema
anatarajia kufungua kampuni ya ujenzi ili mtaji wake uzunguke pamoja na kutoa
ajira kwa vijana mbalimbali wa Kitanzania.
Matarajio mengine
ni kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa ndogo ndogo za
majumbani kama vile juisi, mafuta ya alizeti, mifuko ya plasitik pamoja na maji
ya kunywa kwa ushirikiano na wawekezaji kutoka nje kwa lengo
moja tu la kukuza uchumi wa Tanzania.
Aida
anasema anajihusisha kikamilifu na masuala ya kijamii hasa kusaidia wasiojiweza ikiwemo
yatima lakini mambo hayo huyafanya nyuma ya pazia pasipo kujitangaza.
“Kidogo
nilicho nacho huwa nakitoa kwa wenye mahitaji maalum lakini huwa sijitangazi” anasema.
Maziku ni
kijana wa Kitanzania aliyezaliwa mwaka 1990, kitaaluma yeye ni mtaalamu wa
masuala ya benki na fedha fani ambayo alisoma katika chuo kikuu
cha Zanzibar.
Pia aliwahi kufanya kazi Benki ya Exim kama ofisa wa kawaida wa benki ambayo alidumu nayo kabla
ya kugeukia katika biashara ya mazao.
Maziku ni
mtoto wa mwisho kwenye familia yao yenye watoto
watatu, ndoto yake ni kuwa mfanyabiashara mdogo mwenye mafanikio makubwa kama alivyo Mohammed Dewji(Mo).
Aidha Maziku
anawashauri vijana wenzake wawe na uthubutu kama
aliokuwa nao yeye, aliiona fursa kaichangamkia.
“Vijana
tusibweteke,vikwazo ni vingi,hatupaswi kukata tamaa, hata waliofanikiwa
kama akina Mo hawakuanzia juu, walipambana na uzuri ni kwamba Mo si
mchoyo, ni mtu anayejitoa, mwenye msaada katika mambo mbalimbali ya ushauri wa
kibiashara jambo ambalo linanifanya nimuheshimu na amechangia katika
mafanikio yangu ya kibiashara hivyo sitaacha kumshukuru,” anasema.
Aidha
Maziku anamshukuru rais Jakaya
Kikwete kwa kuwa miongoni mwa watu
waliochangia mafanikio yake.
0658 266
406
Chanzo :Tanzania Daima
Gazeti,August 25,2015
No comments:
Post a Comment