Katibu Mkuu Ofisi
ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi (kushoto) akisikiliza maelezo kuhusu
mradi wa Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji cha Ruhila kilichopo Manispaa
ya Songea mkoani Ruvuma wakati wa ziara ya kukagua shughuli za mazingira leo
Julai 15, 2026.
Na Mwandhi Wetu
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amehimiza wananchi hususan vijana kuchangamkia fursa zinazopatikana kutokana na uhifadhi wa mazingira ili kujipatia kipato.
Dkt. Muyungi ametoa
msisitizo huo alipofanya ziara katika Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji
cha Ruhila kilichopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma leo Julai 15, 2026.
Alisema katika
ziara hiyo amejionea namna mradi huo unavyoweza kuchagiza sekta ya uchumi wa
buluu ambayo Ofisi ya Makamu wa Rais inasimamia kwa kuhamsisha ufugaji wa
samaki ambao huchangia kipato.
Aidha, Dkt.
Muuyungi alieleza kuwa hifadhi endelevu ya mazingira ambayo imechangia kuwepo
kwa mabwawa ya kuzalisha na kufugia samaki katika eneo hilo imegeuka fursa.
“Vijana
wachangamkie fursa hizi za usimamizi wa taka kwani hapa katika kituo hiki
tumeona namna taka hizo zinavyogeuzwa kuwa chakula cha samaki hivyo tusafishe
mazingira yetu tukusanye taka na tuzigeuze fursa, tutapata kipato,” alisema.
Sanjari na hilo
Dkt. Muyungi aliongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Maamu wa Rais katika
utekelezaji wa Dira 2050 ambayo nguzo ya tatu inazungumzia masuala ya hifadhi
ya mazingira, ni hatua mojawapo ya kuhakikisha Sera ya Uchumi wa Buluu inatekelezwa
ipasavyo.
Kwa upande wake Afisa
Mfawidhi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Ruhila Bw. Lucka Mgwena alisema
kituo hicho ambacho kinasimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kinaendelea
kuibua teknolojia rafiki kwa mazingira hasa kwa wafugaji wa samaki.
Alisema utekelezaji
wa mradi huo ni njia mojawapo ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika
kuchagiza sekta ya uchumi wa buluu ambayo imeendelea kukua kwa kasi na kuleta
maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Bw. Mgwena alisema
kupitia mradi huo wafugaji wa samaki wanaweza kupata mbegu (vifaranga) za
samaki ambazo zinazalishwa kwa njia ya kitalaamu na hivyo kuongeza tija katika
sekya hiyo.
“Katika Mkoa wa
Ruvuma kuna kilimo cha vyakula na mazao mbalimbali hivyo tumeibua teknolojia ya
kuzalisha vyakula vya samaki kwa kutumia taka oza kutokana na mabaki ya vyakula
mbalimbali badala ya kuacha taka hizo zikizagaa ovyoo na kuchafua mazingira,”
alisema.






No comments:
Post a Comment