WAKATI ZEC ikitangaza kufuta uchaguzi huo na matokeo yake, Chama cha
Wananchi (CUF) kimeeleza kutotambua uamuzi huo na kuitaka serikali iiache tume
hiyo iendelee na kazi yake ya kuhesabu,
kuhakiki na kutoa matokeo ya uchaguzi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari muda
mfupi baada ya ZEC kutoa tamko hilo,
mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema
ameshtushwa na hatua hiyo inayokwenda kinyume na Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar
na kwamba anaichukulia kauli ya mwenyekiti huyo kuwa ni yake binafsi.
“…hiyo ni kauli binafsi ya mwenyekiti
huyo hasa baada ya kujiridhisha kuwa hakukuwa na kikao chochote cha tume
kilichofikia maamuzi hayo. Mwenyekiti kwa nafasi yake hana mamlaka ya kufuta
uchaguzi huo.
“Inaonekana kuna njama za makusudi
kutaka kuvuruga demokrasia Zanzibar na kuingiza nchi katika machafuko jambo
ambalo sisi kama CUF hatutavumilia,’’alisema Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa
kwanza wa rais na Katibu Mkuu wa CUF, alisema Mwenyekiti huyo wa ZEC
hakutafakari kwamba kuufuta uchaguzi mkuu Zanzibar kunaathiri pia uchaguzi wa
rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu wapigakura ni walewale
waliomo kwenye daftari la wapiga kura la ZEC.
Alieleza kuwa katika kusimamia uchaguzi
huo ZEC hufanya kazi ya uwakala wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na hali hiyo
inaitia Jamhuri ya Muungano katika taharuki bila sababu yoyote ya msingi kwa
sababu rais wa Jamhuri ya Muungano hawezi kupatikana kwa kupigiwa kura na wananchi wa Tanzania Bara pekee.
“Sisi tunatambua hatua hii imekuja
baada ya majaribio yote ya kutaka
kulazimisha ushindi usiokuwepo wa CCM kushindikana. Uhakiki wa matokeo
ya uchaguzi wa majimbo yote 36 ya Unguja
na majimbo manne ya Pemba ulikuwa umekamilika kabla ya zoezi hilo
kusitishwa kuthibitisha matokeo ambayo CUF ilikuwa imekusanya.
“Tunatambua kwamba zilikuwepo njama za
kutaka kumtangaza mgombea urais wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa nguvu lakini
njama hizo zimeshindikana kutokana na
ukweli uliokuwa ukiibuka kupitia uhakiki wa matokeo ya uchaguzi,” alisema na
kuongeza:
“Tunatamka wazi kwamba CUF
hatuutambui uamuzi huo binafsi wa mwenyekiti wa tume na tunaitaka
Serikali ya CCM kuiacha tume iendelee na kazi yake ya uhakiki wa matokeo ya
uchaguzi na kisha kumtangaza mshindi,” alisema.
Waliitaka Jumuiya ya Kimataifa na
marafiki wa Tanzania kuingilia kati suala hilo hasa kwa sababu waangalizi wa
kimataifa wameshuhudia hatua zote pamoja na uhakiki wa matokeo ulivyokuwa
unakwenda.
Alisema CUF imeonekana wazi kwamba ni
mshindi wa uchaguzi wa rais pamoja na majimbo 18 ya Pemba na mengine 9 ya
Unguja, hivyo kuiomba Jumuiya ya Kimataifa isiwaruhusu CCM kukandamiza haki za
kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar kwa mara nyingine tena.
Maalim alisema hawataishia hapo wanaendelea
kufuatilia hilo kwa hatua zaidi kwa kuwasiliana na wahusika mbalimbali ndani na
nje ya nchi, ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo unaotengenezwa huku akiwaomba
wanachama wao kubaki watulivu na kuitunza amani iliyopo.
“Tunawahakikishia kuwa uvumilivu wao
utawapa wanachokitaka na sisi viongozi wao
tutasimamia haki yao kwa njia za amani, lakini za uhakika,” alisema
Maalim Seif. CHANZO GAZETI LA TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment