HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 13, 2015

Msama aanika siri tamasha la Nov.25

Na Francis Dande

WARATIBU wa Tamasha la Muziki wa injili kuombea Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, Kampuni ya Msama Promotions Ltd, wameeleza sababu za kuandaa tamasha jingine la kumshukuru Mungu kwa  kujalia  uchaguzi huo kufanyika kwa amani na utulivu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama (pichani), mwenye uzoefu wa kuratibu matukio ya muziki wa injili tangu mwaka 2000, alisema shukrani kwa Mungu ni jambo muhimu.

“Shukrani ni jambo muhimu sana iwe katika mambo ya kiroho hata yale ya kibinaadamu, hivyo kwa vile tulimuomba Mungu ajalie uchaguzi wetu ufanyike kwa amani na utulivu na ikawa hivyo, hatuna budi kuandaa tamasha jingine la kumshukuru,” alisema Msama.

Msama alisema kama walivyofanya wakati wa kuombea amani na utulivu uchaguzi huo kwa kuwaleta pamoja waimbaji wa kitaifa na kimataifa, ndivyo watakavyofanya katika tamasha hilo la Novemba 25 litakaloanzia jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia mikoani.

Alisema ingawa bado kamati yake inaendelea na mazungumzo na waimbaji mbalimbali, lakini kwa wale wa kimataifa ni kutoka Kenya, Afrika Kusini na DR Congo na wengineo mahiri ambao wataungana na wale wa hapa nyumbani.

Miongoni mwa waimbaji wa kimataifa ambao walipamba tamasha la Oktoba 4 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ni Ephraem Sekereti (Zambia), Sipho Makhabane na Solly Mahlangu (Afrika Kusini), Sarah Kierie wa Kenya na mwingine kutoka Uingereza.

Msama ametumia fursa hiyo kuwashukuru wote waliojitokeza katika katika tamasha la Oktoba 4, pia kushiriki uchaguzi mkuu akiamini kila mmoja alikuwa chachu ya amani ndio maana nchi imevuka salama katika tukio hilo zito ambalo kwa nchi nyingine limekuwa chanzo cha uhasama na mifarakano.

“Kwa kutambua nafasi ya kila mmoja katika kudumisha amani na utulivu, ndio maana sisi Msama Promotions tumeandaa tamasha hili la kutoa shukrani kwa Mungu kutuvusha salama katika tukio
zito la uchaguzi mkuu wa Oktoba 25,” alisema Msama.

Alisema watalitumia tukio hilo pia kuzidi kumsihi Mungu aendelee kuijalia nchi amani na utulivu wakiamini huo ndio mtaji wa maendeleo mbalimbali kwani penye mifarakano ya kijamii, ni vigumu kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo na ikafanikiwa.

No comments:

Post a Comment

Pages