Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akiwa
amembeba mtoto, Haidin Edwin wakati wa hafla ya kukabidhi misaada mbalimbali ikiwemo vyakula kwa vikundi
10 vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu, iliyofanyika jijini
Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. (Picha na Francis Dande)
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama
akiwabidhi watoto Haidin Edwin na Gatson Edwin sehemu ya msaada wa vitu
mbalimbali alivyotoa kwa kikundi cha Tuwakomboe cha Temeke jijini Dar es Salaam
ikiwa ni sehemu ya mapato ya matamasha yaliyopita.
Sehemu ya msaada uliotolewa kwa vikundi 10 vya kulelea
watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Halima
Ramadhani ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Mwandaliwa cha Mbweni Dar es Salaam
akipokea msaada wa vyakula pamoja na mahitaji mengine kutoka kwa Alex Msama.
Watoto
wakipata vinywaji baridi wakati wakisubiri kukabidhiwa msaada wa vitu
mbalimbali kutoka Kampuni ya Msama Promotions.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama
Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari.
Dar es Salaam, Tanzania
KAMPUNI ya Msama Promotions ya jijini
Dar es Salaam chini ya Mkurugenzi wake, Alex Msama, ilikabidhi misaada ya vitu
mbalimbali kwa vituo 10 vya kulea watoto yatima ikiwa ni sehemu ya mapato ya
matamasha yaliyopita.
Akikabidhi misaada hiyo kwa watoto
hao, Msama alisema wamefanya hivyo kwa kutambua nafasi yao katika jamii kwamba,
watoto hao wanayo haki ya kupata mahitaji muhimu katika makuzi kama wengine
wenye wazazi wao.
Msama alisema msaada huo wenye
thamani ya sh. milioni 7.5, ni sehemu ya fedha ambazo zimekuwa zikipatikana
kupitia matamasha ya muziki wa Injili ambayo ni wakati wa Pasaka na Krismasi.
“Msaada huu ni sehemu ya fedha ambazo
tumekuwa tukizipata kwa njia ya matamasha ambayo tumekuwa tukifanya jijini Dar
es Salaam na mikoani; Pasaka na Krismasi,” alisema.
Msama, alisema wamekuwa wakisaidia
watoto yatima na makundi mengine maalumu katika jamii kwa kutambua kuwa huo ni
wajibu wa kila mmoja na ametoa wito kwa wengine kuwa na moyo wa kusaidia
makundi hayo.
Vituo vilivyopata misaada hiyo ni
Umra, Zaidia, Hiari, Malaika, Maunga, Mwandaliwa, Sifa, Honoratha,
Chakuwama na Rahman vya jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa vitu vilivyokabidhiwa ni
unga wa sembe, mchele, unga wa ngano, sukari, sabuni, mafuta ya kupikia, mafuta
ya kupaka, dawa za meno na vinginevyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
baada ya kupokea misaada hiyo ya kiutu, viongozi wa vituo hivyo walisema ni
faraja kubwa kwao na watoto hao wenye mahitaji maalumu.
Maombio Jonas, mwakilishi wa Kituo
cha Sifa Group Foundation cha Bunju, ametoa shukrani kwa Msama kwa moyo wa
kujitolea kusaidia watoto wenye mahitaji na kutoa wito kwa wengine kuiga mfano
wa moyo huo wa upendo.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Hiari
cha Chang’ombe, Aminajat Klemia, alitoa pongezi kwa Msama kutokana na misaada
hiyo akisema ni faraja kubwa kwa watoto hao ambao wanahitaji kuthaminiwa kama
wengine.
Misaada hiyo imetolewa wakati ambapo
kampuni hiyo ipo katika maandalizi ya Tamasha la Krimasi litakalofanyika
Desemba 25 kwa ajili ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo pia kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kuijalia nchi kuvuka salama katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
25.
No comments:
Post a Comment