Jengo la
tatu la abiria (TB III) linalojengwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNIA), Jijini Dar es Salaam limekamilika kwa asilimia 65 na
linavutia.
Jengo hilo
lenye uwezo wa kuchukua abiria milioni 6 kwa mwaka limewavutia wahandisi
ujenzi kutoka mkoa wa Pwani waliolizuru
leo na wadau wa usafiri wa anga jana.
Akizungumza
kwa niaba ya Wahandisi wenzake leo, Mhandisi Michael Mrema amesema, mradi huo
ni mkubwa, mzuri na wenye tija kwa uchumi wa nchi na kwamba wamefurahi kupata
nafasi ya kujifunza ulivyo.
Meneja Mradi
wa Bam International ya Uholanzi inayojenga jengo hilo, Eric Van Zuthem amesema
leo, wamefurahi kupata fursa ya kuwajengea Watanzania hasa wadau wa usafiri wa
anga jengo hilo la aina yake.
“Jengo hili
litakuwa la kimataifa kutokana na vifaa vya usalama vitakavyofungwa hasa
ukizingatia hivi sasa kuna matukio ya ugaidi kama yaliyotokea Ufaransa
karibuni. Ni furaha kufanya kazi na TAA na wadau pia kuwajengea Watanzania, jengo
zuri litakalovutia wageni.’ amesema.
Mkurugenzi
wa Mradi wa TB III, Mhandisi Mohammed Millanga amesema, mradi huo unaotekelezwa
kwa awamu mbili, utakamilika mwaka 2017. Amesema awamu ya kwanza inatarajiwa
kukamilika Juni 2016.
Amewaeleza
Wahandisi hao kuwa Mkandarasi, Bam International alipewa zabuni moja ya kujenga
kwa awamu mbili ambapo awamu ya pili inatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya
Serikali kuridhia kutolewa fedha.
Amewaeleza wahandisi hao jengo hilo linajengwa kwa gharama ya
Euro milioni 235 (sh. Bilioni 518). Awamu ya kwanza inagharimu Euro milioni
133.2 (sh. Bilioni 293) na ile ya pili itagharimu Euro milioni 102 (sh. Bilioni
225).
Kati ya fedha hizo, asilimia 85 inagharamiwa na Benki ya HBSC
ya Uingereza kupitia mkopo unaodhaminiwa na Serikali ya Uholanzi na asilimia 15
Benki ya CRDB za mkopo unaodhaminiwa na Serikali ya Tanzania. Tayari Uholanzi
imetoa fedha za awamu ya pili ili kazi ianze.
Mbali ya kuchukua abiria milioni 6, jengo hilo litakuwa na
miundombinu ya madaraja makubwa ya abiria matano ya kuegesha ndege 18 na ndege
moja kubwa aina ya Airbus 380. Pia
litakuwa na migahawa, sehemu za kusali, watoto kucheza na theluthi moja
yake ni sehemu za biashara.
Jana wadau
kutoka mashirika ya ndege, wauza tiketi za ndege, wauzaji vifaa vya ujenzi,
mawakala wa mizigo ikiwemo Swissport, maofisa ubalozi walizuru jengo hilo na
kusifu ubora wake, miundombinu na viwango vyake.
Kutokana na
abiria wanaotarajiwa kuongezeka baada ya jengo hilo kukamilika, Mhandisi
Millanga amesema TAA inafikiria kuongeza njia za kurukia ndege ziwe mbili ili
kukidhi mahitaji ya ongezeko la ndege zirukazo JNIA.
Amesema TAA
inafikiria kuongeza njia hiyo ili moja itumiwe na ndege ndogo tu na nyingine
kubwa. Kwa sasa JNIA ina njia moja ya kurukia ndege na abiria wanaopita jengo
la pili la abiria, wanakadiriwa kuwa milioni 2.5.
No comments:
Post a Comment