HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 18, 2015

Wakorintho wa Pili, wajitosa Tamasha la shukrani Diamond

NA MWANDISHI WETU

KWAYA  ya  Wakorintho  wa Pili ya Wilayani Mafinga mkoani Njombe, imekuwa ya kwanza  kuthibitisha kushiriki Tamasha la Kushukuru linalotarajia kufanyika Desemba 25 katika  ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Hayo yalidokezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo la aina yake, Alex Msama, wakati akizungumzia maandalizi ya kulifanya tamasha hilo linabeba uzito wa aina mbili kwa pamoja; Krismas na shukrani.

Alisema kwa vile wamekuwa wakiratibu tamasha la Krismas kila mwaka, hivyo safari hii tamasha hilo litakuwa na uzito zaidi kwani litawaleta wengi kufurahia kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, pia kumshukuru Mungu nchi kuvuka salama uchaguzi mkuu.

“Tamasha hilo litakuwa la aina yake, litabeba uzito wa shukrani kwa Mungu kwa kuijalia nchi kuvuka salama katika uchaguzi mkuu uliokuwa na ushindani mkubwa, pia kuwaleta wapendwa pamoja kuifurahia krismas,” alisema Msama.

Kuhusu suala la waimbaji, Msama alisema uongozi wa kwaya ya Wakorintho wa Pili, umekubali kushiriki tamasha hilo wakiungana na wengine watakaopata fursa ya kushiriki kwa lengo la  kumshukuru Mungu na kuutukuza ufalme na ukuu wake.

“Kwaya  ya Wakorintho wa pili  wameanza kuthibitisha kushiriki tamasha la Shukrani baada ya kufanyika uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu, tunaendelea na maandalizi ya kufanikisha tamasha hilo ambalo litashirikisha idadi kubwa ya Watanzania,” alisema Msama. 

Msama aliongeza kuwa Kwaya hiyo italitumia Tamasha hilo kufanya uzinduzi wa albamu yake ya Mchepuko sio Dili yenye jumla ya nyimbo nane.

Nyimbo zilizoko kwenye albamu ya Mchepuko sio dili ni pamoja na Tanzania, Mchepuko sio dili, Watenda mabaya, Eee bwana, Tuokoe baba, Dunia hii, Yahwe Tunakuinua na Hana. 

“Kwaya  ya Wakorintho itafanya matukio mawili katika tamasha hilo, la kwanza ni kushiriki Tamasha la Kushukuru na la pili ni kuzindua albamu yenye nyimbo nane,” alisema Msama.

No comments:

Post a Comment

Pages