Haihitaji
kuwa na akili sana ili kuiona tofauti ya maisha kati ya miji iliyoendelea na
vijijini. Hapa nazungumzia ushirikiano wa wakazi wa maeneo hayo mawili na viongozi
wao wa serikali hasa kuanzia ngazi ya mtaa na kata.
Majadiliano yakiwa yanaendelea |
Wakazi
wengi wa mijini huwa wanabanwa na shughuli mbalimbali za kujitafutia kipato
kiasi kwamba hukosa hata nafasi ya kuwafahamu viongozi wa serikali ya mtaa wao.
Aina hii ya maisha hupelekea kuzaliwa kwa tabia mbaya zaidi, nayo ni kukosa
muda wa kuhudhuria mikutano muhimu inavyofanyika katika mitaa yao.
Hali
hii ni tofauti kwa vijijini ambapo wananchi wengi mwenendo wa maisha yao ya
kila siku kutoka kwa viongozi wao kuanzia ngazi ya kijiji, kitongoji na kata.
Kutokana na aina hii ya maisha inawafanya wawe na umoja, kuishi kwa ushirikiano
na kufanya maamuzi kwa pamoja hasa juu ya rasilimali zao.
Katika
miaka ya hivi karibuni wanakijiji wengi wanaoishi katika maeneo yenye
rasilimali wametambua umuhimu wa kutunza na kutumia rasilimali zao vizuri kwa
maendeleo yao na kwa manufaa ya vizazi vijavyo. Lakini si kila sehemu hali ipo
hivyo katika baadhi ya maeneo wanakijiji wamekuwa hawazitambui haki zao za
msingi kutokana na uelewa mdogo.
Mwalimu kaziro Nyangisa akisoma moja ya mikataba |
Mwime
ni kijiji kilichopo katika kata ya Mwendakulima wilayani Kahama, mkoani
Shinyanga. Wakazi wengi wa kijiji hiki ni wakulima wadogo wadogo, wafugaji na
ni wachimbaji wa madini.
Kijiji
hiki ndicho kilichohifadhi mgodi maarufu wa dhahabu wa Buzwagi, uliochangia kwa
kiasi kikubwa kupanda kwa hadhi ya kijiji hicho na kuwa mtaa. Hivyo kwa sasa
Mwime ipo kwenye halmashauri ya mji kutokana na upatikanaji wa huduma muhimu
karibia zote kuanzia huduma za afya, barabara, umeme na maji safi.
Awali
kijiji cha Mwime kilikuwa kikimiliki leseni mbili za machimbo ya uchimbaji
dhahabu ya Majimaji na Zanzibar. Wachimbaji wadogo wadogo walikuwa ndio
walengwa wakubwa, ambapo walilipa ushuru kwa serikali ya kijiji. Na wao
kunufaika na shughuli hizo ambazo zilikuwa zinawaingizia kipato.
Uraghbishi umesaidia kupata Barabara nzuri |
Ilipofika
mwaka 2007 kampuni ya Pangea ilipata leseni ya kufanya utafiti na mwisho wa
siku kuingia mkataba na serikali ya kijiji cha Mwime. Katika kipindi ambacho
uwekezaji ulikuwa unafanywa katika eneo hilo ambalo sasa ni mgodi wa Buzwagi,
kijiji kililipwa kiasi cha shilingi za kitanzania 12,000,000 kwa mwaka ikiwa
kama malipo ya kusitisha uchimbaji katika eneo hilo.
Uraghbishi umesaidia kuleta umeme katika mtaa wa Mwime |
Miaka
miwili baadaye yaani mwaka 2009, ndipo kijiji kilipokabidhi rasmi leseni zake
kwa kamishina wa madini na kuingia mkataba na Pangea (Barrick). Kwa mujibu wa kifungu namba 1.1 cha Makubaliano ya Nyongeza ya Mkataba
baina ya Kampuni ya Madini ya Pangea (Barrick) na Kijiji cha Mwime; kampuni
itakuwa ikikilipa kijiji kiasi cha Tsh milioni 60/- kila mwaka kwa kipindi cha
miaka mitano na kisha pande mbili hizi zitakaa pamoja na kupitia kiwango hiki
kwa kadri ya uzalishaji utakavyokuwa kwa nia ya kuboresha zaidi.
Hizi ni Nyumba mbili zilizojengwa kwa ajili ya walimu |
Malipo haya yalitakiwa kuanza kulipwa kuanzia mwaka
2009 miaka miwili baada ya makubaliano kusainiwa tarehe 21 mwezi Aprili mwaka
2007. Ni mwaka 2012 malipo haya yamelipwa kwenye akaunti ya kijiji, kiasi hicho
cha shilingi milioni 300/- ni malipo ya miaka mitano ya awamu ya kwanza;
mkataba unatamka kila baada ya miaka 5 pande mbili (Kijiji na Mgodi) zitakaa
kupitia kiwango hiki ili kuboresha kiwango hiki kutegemeana na uzalishaji.
Malipo haya yanafanyika, baada ya juhudi kubwa kufanywa
na wananchi wa kijiji cha Mwime na viongozi wao katika kufuatilia fedha hizo.
Na tatizo halikuwa upande wa mgodi wa Buzwagi, bali ni wananchi wa kijiji cha
Mwime wenyewe kushindwa
kuhimiza uongozi wao kuchukua hatua za kufuatilia suala hilo. Na hivyo kupita
miaka miwili bila kitu chochote kufanyika kuanzia 2009 hadi 2011.
Hizi ni nyumba mbili ambazo zimejengwa kwa ajili ya wauguzi |
Kwa
mujibu wa kifungu cha 1.2 cha Nyongeza ya Mkataba wa Makubaliano, fedha
zitakuwa zinalipwa kupitia Bodi ya Wadhamini, ambayo inaundwa na wawakilishi wa
kijiji, mgodi na serikali ngazi ya wilaya kama msimamizi.
“Lilitolewa
tangazo kwa ajili ya watu kuomba nafasi ya kuwa wawakilishi wa kijiji kwenye
Bodi, ila waliotakiwa ni wale walio chini ya miaka 60 na waliomaliza kidato cha
nne. Nilipata hisia kwamba tangazo limebagua baadhi yetu wenye uwezo ila hatuna
sifa walizozitaja,” anaelezea Maimuna Said mmoja wa waraghabishi wa kijiji hiko.
Wanakijiji wa Mwime pia wanafanya shughuli za kilimo na ufugaji |
Hivyo wakati wa mkutano wa kijiji mwaka 2011
wanakijiji walitaka maelezo ya ziada kuhusu uundwaji wa Bodi ya Wadhamini
pamoja na majukumu yake. Ndipo ilipojulikana kwamba tayari kuna watu
wameshaomba nafasi hiyo na tayari wameshachanguliwa na zaidi Bodi hiyo ina
mamlaka ya mwisho ya kuamua matumizi ya fedha itakazolipwa kijiji.
Uraghbishi
huo ulipelekea kamati iliyokuwepo kuvunjwa na wanakijiji walioamua kuchagua
viongozi wao wanaowataka na kupelekea kupata malipo yao vizuri na kufanyia
maendeleo ya kijiji. Jitihada hizo zilimvutia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo,
Lembeli kuchangia fedha kwa ajili ya kufungua akaunti ya kijiji ya maendeleo.
Sehemu
ya fedha hizo (milioni 300/-) zilitumika katika kufungua miradi ya maendeleo
ikiwa ni pamoja na Tsh 78,000,000 kutumika kujenga nyumba mbili za kuishi
wauguzi, kuvuta umeme kijijini hapo na kujenga barabara huku Tsh 7,000,000 zikitumika
kulipa fidia kwa watu waliokuwa na miti na makaburi sehemu ambayo barabara hiyo
ilipita.
Mbali
na hayo Tsh 1,800,000 zilitumika kuwalipa posho wafanyakazi wote walioshiriki
kufanya kazi hiyo, yote hayo yaliweza kufanikiwa kutokana na kazi kubwa
iliyofanywa na walaghabishi.
Mgodi umesaidia hata wanakijiji kuwa na vitega uchumi vyao wenyewe |
Waraghbishi
mwalimu Kaziro Nyaingisa na mkulima Maimuna Said, wakirishirikiana na wanakijiji
cha Mwime kupitia kamati iliyochaguliwa kupigania mkataba mpya na kampuni ya Accacia
iliyowekeza kwenye mgodi huo baada ya Barrick. Katika mkataba mpya wa mwaka
2015/2016 umeongezeka kwa asilimia 50% kutoka Tsh 60,000,000 kwa mwaka mpaka
kufikia Tsh 90,000,000 ambapo mpaka sasa fedha hizo zimeshaingia kwenye kamati
na zinaendelea kutatua matatizo ya kijiji.
Kama
hiyo haitoshi, Uraghbishi huo umewafanya wawekezaji wa mgodi wa Accacia kutoa
ajira za utunzaji wa mazingira kwa wanawake ambao wanaishi jirani na mgodi,
huku wakitengeneza matundu ya vyoo vya kisasa 16 kwa ajili ya wanafunzi wa
shule ya msingi Mwime. Wameahidi pia kuongeza idadi ya visima vya pete na nyumba
za walimu.
Kutokana
na waraghbishi kupaza sauti zao imewasaidia wanakijiji hasa raia wa kawaida
kuwa na uwezo mkubwa wa kujitambua, kujua haki zao na uhalisia katika jamii. Wametambua
nini maana ya uzalendo, umuhimu wa ushirikiano, watu kuishi kwa amani, na kufanya
kazi bila woga.
Kupitia
uraghbishi wanawake wamekuwa sio waoga tena katika kijiji cha Mwime, hiyo
imesababisha mpaka vijiji vingine kama Kilago na Nyandekwa.
(Imeandaliwa na Fredy Njeje wa Blogs za Mikoa)
No comments:
Post a Comment