Mwenyekiti wa Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste (Tanzania Fellowship of Churches) Askofu Godfrey Malassy akionyesha kitabu mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kilichozinduliwa na Jumuiya ya Makanisa hayo kinachohusu siri ya amani kwa taifa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste (Tanzania Fellowship of Churches) Askofu Godfrey Malassypa (kushoto) pamoja na Mwanakamati wa Jumuiya hiyo, Mchungaji Olivia Mallonga wakiomba mara baada ya kukamilika kwa mkutano na waandishi wa habari leo 22 Desemba, 2015 katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Benedict Liwenga)
Na Shamimu Nyaki
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkesha mkubwa wa kuiombea amani Tanzania utakaofanyika Disemba 31 mwaka huu katika uwanja wa Taifa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Makanisa ya Pentekoste (TFC) Godfrey Malassy alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijin Dar es Salaam, na kuthibitisha kuwa maandalizi yote yamekamilika ikiwemo kibali kutoka polisi, pamoja washiriki mbalimbali watakaoshiriki katika mkesha huo.
Askofu Malassy ameongeza kuwa mkesha huo utakuwa ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuijalia nchi yetu kumaliza Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka huu kwa amani na utulivu,pamoja na Dua maalum ya kumuombea Mhe. Rais afya njema na utendaji mzuri anaoendelea kuufanya kwa maendeleo ya Taifa letu kwa kuwa mara zote amesisitiza kufanyiwa maombi na watanzania.
“Tutatumia nafasi hiyo kumuombea Mhe.Rais katika kutekeleza jukumu kubwa alilokabidhiwa na watanzania kuongoza Taifa letu ili aweze kufanikiwa katika hilo.”Alisema Askofu Malassy.
Aidha Mwenyekiti huyo amewataka wananchi wote kutumia siku hiyo kumuomba na kumshukuru Mungu kwa amani iliyopo nchini kwa vile ndio msingi mkubwa wa shughuli za kila siku zinazosaidia kupata kipato na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Naye Mch.Olivia Mallonga ambaye ni mjumbe katika kamati ya maandalizi ya Mkesha huo amesema kwamba wao kama wadau wanaendeleza desturi ya kuliombea Taifa amani ili lisije kutumbukia kwenye machafuko kama nchi nyingine .
“Watanzania wana dini ndio maana wanatumia imani zao kufanya maombi ili Mungu awalinde na maovu au machafuko yanayoweza kutokea kutokana na sababu yoyote.”Aliongeza Mch. Olivia.
Mkesha huo ni wa 17 tangu ulipoanza kufanyika Tanzania na umeleta mafanikio makubwa ikiwemo kuunganisha watanzania bila kujali imani zao.
No comments:
Post a Comment