Kufuatia taarifa ya tahadhari ya uwezekano wa kuwepo kwa
mvua za El-Nino iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Mwezi Agosti 2015, Ofisi
ya Waziri Mkuu ilitoa agizo kwa Mikoa yote nchini kuchukua hatua za kujiandaa
na kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo. Kamati za
Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji ambazo ndizo zenye jukumu kubwa la
kusimamia masuala haya,
hazijatekeleza agizo hilo kwa kuainisha hatua
zilizochukuliwa katika Kuzuia/Kupunguza, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali
baada ya maafa kutokea. Hivyo;
“Naagiza wenyeviti
wa kamati za maafa katika ngazi husika kwa kushirikiana na taasisi na idara za
serikali zinazohusika waorodheshe watu wote wanaoishi katika maeneo hatarishi
na kuwapa barua za kuwataka kuhama mara moja katika maeneo hatarishi ili
kuepuka athari za maafa. Taarifa za utekelezaji wa agizo
hili ziwasilishwe katika Ofisi ya Waziri Mkuu haraka sana kadri iwezekanavyo” amesema
Mhe. Mhagama.
Ili kutekeleza agizo hili ninaziagiza Kamati za maafa za
Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji ziwajibike kutekeleza mambo yafuatayo;
I.
Kamati zote ambazo
hazijatekeleza maagizo yaliyotolewa na viongozi katika kushughulikia maafa
zitoe maelezo ya kwanini hazijatekeleza maagizo hayo kwa mamlaka husika.
II.
Endapo kutatokea maafa
mahali popote katika nchi yetu kwa sasa, kamati za maafa zitawajibika kuelezea
sababu za kutokea kwa maafa hayo ni nini katika maeneo yao na kuainisha hatua
zilizochukuliwa na kamati hizo za kukabili hali hiyo iliyojitokeza.
Lakini
taarifa hizo pamoja na kuwasilishwa kwenye mamlaka husika pia ziwasilishwe
kwenye vyombo vya habari.
III.
Kamati zote za maafa katika
ngazi zote, zitoe maelezo na mipango waliyonayo juu ya kupambana na mlipuko wa
ugonjwa wa kipindupindu janga ambalo linasababisha maafa katika nchi yetu.
IV.
Kamati zote za maafa katika
ngazi zote, zishirikishe wadau wa maafa (Wananchi, Taasisi na Sekta binafsi) katika
mipango yao yote ya kukabili maafa ya menejimenti ya maafa.
V.
Kamati zote za maafa
ziendelee kuratibu na kutoa taarifa juu ya misaada yote ya maafa inayotolewa na
Serikali pamoja na wadau katika kusaidia waathirika wa maafa pale yanapotokea.
VI.
Kamati hizo za maafa katika
ngazi zote zinatakiwa, kuchukua /kumchukulia hatua mtendaji na mhusika mwingine
yeyote ambaye hatatimiza wajibu wake na kutotekeleza maagizo yanayotolewa na
viongozi nchini katika kukabili maafa mahali popote.
“Serikali inawaomba wadau wote wa maafa
ushirikiano wa hali ya juu katika jambo hili muhimu katika nchi yetu ili kuweza
kuokoa watanzania wengi ambao wanaweza kukumbwa na maafa kwa namna moja ana
nyingine”, amesisitiza Mhagama
Aidha, Sheria Na. 7 ya Mwaka 2015 ya Menejimenti ya Maafa
inamtaka kila mdau kutekeleza wajibu wake katika suala zima la menejimenti ya
maafa ikiwa pamoja na Kuzuia, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali baada ya
maafa kutokea.
“Napenda kuchukua
fursa hii kuzikumbusha Kamati za maafa katika ngazi za Mikoa, Wilaya,Kata na
Vijiji kuhakikisha kuwa zinatimiza wajibu wao katika suala zima la
kushughulikia maafa kwa mujibu wa sheria” amesema Mhe. Mhagama.
Hivi sasa sehemu mbalimbali za nchi yetu zimekuwa zikipata
mvua nyingi ambazo zimesababisha maafa na baadhi ya sehemu zinakabiliwa na
ukame.
Taarifa nyingi zilizopokelewa zinaonesha baadhi ya maeneo
ya nchi yetu yamekuwa yakipata mvua nyingi ambazo zimesababisha maafa bila Kamati
za Maafa za Mikoa, Wilaya,Kata na Vijiji kuainisha hatua zilizochukuliwa katika
Kuzuia/Kupunguza, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
Iwapo juhudi za ngazi zote pamoja na Mkoa zitashindwa
kukabili maafa yanayotokea katika ngazi za Wilaya, Kata na Vijiji, taarifa na
maombi zitumwe katika ngazi ya Taifa kwa kuzingatia maelekezo/mwongozo wa
uombaji wa misaada na utoaji wa taarifa za maafa uliotolewa na Ofisi ya Waziri
Mkuu.
Imetolewa na
JENISTA
J. MHAGAMA (MB)
WAZIRI WA NCHI OFISI YA
WAZIRI MKUU
SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA
NA WATU WENYE ULEMAVU
22 DESEMBA 2015
No comments:
Post a Comment