HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 02, 2015

RC Makalla atembelea kiwanda cha sukari TPC

RC Makalla atembelea kiwanda cha sukari TPC, akerwa na sukari inayoingia kwa wingi kutoka nje

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Amos Makalla akiwa kwenye ukaguzi wa kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Moshi, mkoani humo, kama sehemu ya kuangalia hali ya uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho. Picha na Mpigapicha wetu.

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

MKUU wa Mkoa Kilimanjaro, Amos Makalla, amefanya ziara katika kiwanda cha Sukari cha TPC kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro ili kujionea hali ya uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho. RC Makalla alijionea hali halisi ya kiwanda hicho ambacho sasa kinazalisha sukari tani 105,000 baada ya kubinafsishwa, tofauti na uzalishaji wa tani 35,000 tu hapo zamani.
Ziara inaendelea kiwandani hapo.
Akizungumza katika kiwanda hicho, RC Makalla alisema kwamba amefurahishwa na hali ya uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho, huku akiahidi kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Tanga kudhibiti sukari inayoingia kutoka nje ya nchi. Alisema atashirikiana na serikali ya Mkoa wa Tanga kudhibiti sukari hiyo ya nje, akiamini kuwa kutasababisha kiwanda hicho kupiga hatua kwa kuuza sukari yao nchini.
Majadiliano yanaendelea kiwandani hapo dhidi ya RC Makalla
“Kilio cha kiwanda hiki ni uingizwaji wa sukari kutoka nje, hivyo Kilimanjaro tutashirikiana kwa karibu na wenzetu wa Tanga ili kuweka ulinzi mkali kwa ajili ya kudhibiti sukari inayoingia kutoka nje kwa kupitia mkoani Tanga.

“Naamini tukifanya hivyo tutaweza kukiweka kiwanda hiki katika hali nzuri, ukizingatia kuwa viwanda vyetu ili viweze kujiendesha vinapaswa kuuza bidhaa zao vizuri na si kupata changamoto zinazoweza kuwaathiri kama suala hili la sukari nyingi kuingia kutoka nje wakati wao pia ni wazalishaji,” alisema Makalla.

Kwa wiki kadhaa sasa RC Makalla amekuwa akifanya ziara mbalimbali mkoani Kilimanjaro pamoja na kufanya vikao muhimu vyenye lengo la kuhakikisha kwamba wanaenda mchaka mchaka ili kwenda sambamba na kauli ya hapa kazi ya Dr John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Pages