SIKU
moja baada ya Serikali kutangaza kuchukua hatua za kupunguza riba za mabenki
kwa wananchi kwa kuagiza akaunti za mashirika na taasisi zake katika mabenki ya
kibiashara zifungwe na kuhamisha fedha zilizopo katika akaunti hizo kwenda
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), benki ya CRDB imeunga mkono hatua hiyo.
Pia
benki hiyo imewataka wananchi wasiwe na hofu juu ya mpango huo, kutokana na
hofu iliyojengeka kwamba kuna hatari benki za kibiashara kufilisika nchini.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles
Kimei alisema uamuzi uliofanywa na Serikali utasaidia kukuza uchumi pamoja na
kutambua fedha zake mahali zilipo.
Alisema
Serikali ina haki na nia njema kwa kutaka akaunti hizo zifunguliwe BoT kwa kuwa
zimekuwa zikifunguliwa kwenye mabenki makubwa ya kibiashara, huku baadhi ya Wakala
wa ukusanyaji wa fedha wakishindwa kuzifikisha serikali kama inavyotakiwa.
Pia
alieleza kuwa mfumo huo hauna utofauti na awali kwani utofauti utakuwepo
kutokana na mashirika na taasisi kufungua akaunti BoT, ambapo lengo kubwa ni walaka
wa Hazina kulenga kuboresha mapato ya serikali ammbayo yanaweza kutumiwa kwa
namna mbalimbali.
“Mfumo
huu…utakuwa hauna tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa fedha zitakazokuwa zikiingizwa
kwenye akaunti hizo ni zile zilizokuwa zikiingizwa kwenye benki awali, ili kupunguza
kiwango cha riba,”alisema.
Pia
alisema hofu nyingine inayojengeka kwa wananchi inatokana na mfumo huo
kutotumiwa kwa muda mrefu na BoT, licha ya kuwa kuna baadhi ya nchi inatumia
mfumo huo na hakuna madhara yoyote.
“Hivyo
tunafikiri maamuzi hayo hayana athari zozote kwani nchi mbalimbali zimekuwa
zikitumia mfumo huo ikiwemo Uganda, Rwanda na Kenya ila kwa kwetu unaonekana
mgeni kutokana na kutotumika kwa muda mrefu,”alisema.
Pia
Dk.Kimei kuwa kutokana na uwepo wa mfumo huo benki za kibiashara zitawakopesha
zaidi sekta binafsi, ikiwa tofauti na malalamiko ya mwanzo kwamba Serikali
inapata manufaa kutokana na kukopeshwa zaidi.
“Hii
itasaidia hata wananchi wa kiwango cha chini kuchukua mikopo kutokana na riba
kuwa ndogo, ambapo hata wananchi wa chini wataweza kuchukua mkopo, ikiwa
tofauti na awali wananchi wanashindwa kuchukua mikopo kutokana na riba kuonekaa
kuwa juu zaidi ya asilimia 10,”alisema.
Mbali na
hilo, pia Kimei alisema endapo riba ikiwa inapungua itasaidia kukuza uchumi
kutokana na wananchi wengi wa hali ya chini kuchukua mikopo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam leo, kuhusu serikali kuhamishia akaunti zote za mapato Benki
Kuu. Kulia ni Mkurugenzi wa Hazina wa Benki ya CRDB, Alex Ngusaru na Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja, Tully Mwambapa.
Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja, Tully Mwambapa (kushoto) akizungumza katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja, Tully Mwambapa (kushoto), Mkurugenzi wa Hazina wa Benki ya CRDB, Alex Ngusaru na Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya CRDB, Philip Alfred wakiwa katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment