HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 10, 2016

WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA KATIKA UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR

Na Talib Ussi, Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar (SMZ) imesema uchaguzi wa marejeo uko pale pale licha ya baadhi ya waangalizi wa kimataifa kusema hawatoshiriki uchaguzi huo.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Muhammed alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwa Vuga Mjini hapa.

Alisema wao hawataacha kufanya shuhuli yao eti kwa sababu hakuja mtu Fulani kushuhudia.

“Sisi hatujawahi kutuma watu kwenda kuingilia uchaguzi wa Marekeni kwa hiyo na sisi hatuoni haja tusiendelee na shuhuli yetu” alisema Mohammed.

Alisema wanavyoamini uchaguzi umefutwa na Tume ya Uchaguzi iliyohuru kwa hiyo hawana budi kukubali maamuzi ya ZEC.

“Tume yetu ipo kikatiba na haingiliwi kwa mujibu wa katiba lazima tuheshimu maamuzi yake” alieleza Mohammed.
Sambamba na hilo waziri huyo alisema SmZ itahakikisha amani na utulivu ulio mkubwa unakuwepo kwenye uchaguzi huo.

Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi bila woga kwenda kufanya maamuzi yao kwa kuchagua viongozi wanao wataka.
“Maamuzi ya wananchi yataheshimiwa kwa mujibu wa sheria ziliopo” alisema Mohammed.

Siku za hivi karibuni Jumuiya ya Ulaya na Marekani walitangaza wazi kwamba hawatashiriki uchaguzi huo wa marejeo kwa kile walichosema kwamba ni batili.

Ama kwa upande wa JWTZ na Vikosi vya SMZ kufanya mazoezi na kutembea na vifaru mitaani kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi huo, alisema hayo ni mazoezi yao ya kawaida kuwataka wananchi kuondoa ghofu.

Alisema mara nyingi inapofika wakati kama huu JWTZ na Vikosi vya SMZ hufanya mazoezi yao na kuambatana na matembezi ya maeneo tofauti lakini mwaka huu yamesadifiana na uchaguzi wa marejeo.

Hivi sasa JWTZ pamoja na vokosi vya SMZ vinapita mabarabarani vikiwa na magari maji kuwasha na vifaru katika maeneo yote ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Pages