HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 07, 2016

WAWAKILISHI ZANZIBAR WATAKA AHADI ZA RAIS ZITEKELEZWE


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

 
WAJUMBE  wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameitaka Ikulu kuhakikisha ahadi za rais zinatekelezwa kwa wakati muafaka ili kufikia malengo yaliykusudiwa.
 

Akizungumza wakati akichagia hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyoitoa wakati akizindua Baraza la Tisa, Mwakilishi wa Jimbo la  Uzini, Muhammed Raza Dharams, alisema mara nyingi rais anapokwenda katika kazi za kuzindua skuli au hospitali,  gharama za mapambo ni zaidi Sh. Milioni 20.
 

“Lakini rais akitoa hadi ya milioni mbili tu basi, inawezekana kuchukua miaka yote mitano haijatimizwa ahadi hiyo,” alisema Raza.
 

Alisema ni vema watendaji wakawajibika ipasavyo na kufanya majukumu yao kwa mujibu wa maelekezo waliyopewa ili maendeleo ya nchi yaweze kuonekana.
 

“Mimi nina ushahidi, akienda sehemu rais, basi hutafutwa tajiri akaambiwa toa milioni 20 haraka haraka, lakini subiri hiyo ahadi, hapo ndiyo balaa,” alieleza Raza.
 

Kwa upande wake Mwakilishi wa kuteuliwa na Rais, Hamad Rashid Muhammed, aliwaomba viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenda na wakati na kuacha kulewa  mazoea.

“Viongozi wetu hawana uwajibikaji ambao unatakiwa hasa katika kipindi hiki kigumu tunachoelekea” alieleza Muhammed.
 

Alisema kama watajitahidi kukusanya mapato na yakatumiwa
kwa kinachokusudiwa, basi hakutakuwa na haja ya kutegemea wahisani ambao wanadai kuzuia misaada yao.

“Tufanyeni kazi kwa manufaa ya nchi yetu na si kwa matakwa ya mtu binafsi ili maendeleo yetu yaonekane,” alieleza Muhammed.

Aidha, kwa upande wa mwakilishi wa Jimbo la Kijito Upele, Ali Suleiman Ali, alisema kama viongozi wa SMZ watafanya kazi kwa nia njema, maendeleo yanaweza kuonekana.
 

“Tumeshasikia Marekani na wenzake wameshaaza kuzuia misaada yao kwetu, sasa tuchangamkeni na watakaochaguliwa mawaziri washuke hata mabondeni,” alisema Ali wakati akichangia hotuba ya Rais wa Zanzibar.
 

Baraza hilo la wawakilishi linaloendelea hapa litegemewa kuahirishwa Ijumaa ijayo baada ya wajumbe wote kupata fursa ya kuchangia hotuba hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages