WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhiwa maabara ya kitabibu
inayoweza kubebwa kwenye sanduku (Mobile and Compact
Portable Clinical Laboratory) ambayo ni rahisi
kutumika mahali popote hata kwenye maeneo yasiyo na umeme.
Maabara hiyo ambayo inatumia umeme wa mionzi ya jua inaweza
pia kuchajiwa na betri ambayo inawashwa na umeme wa kwenye gari.
Akitoa maelezo mbele ya Waziri Mkuu jana (Jumanne,
Julai 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni ya ACCUSTER ya India, Bw. Amit Bhatnagar alisema maabara
hiyo imeundwa kwa lengo la kusaidia kupunguza tatizo la umbali kwa wananchi
waishio vijijini.
“Jumla ya taasisi za kijamii 100 nchini India
zimekwishanunua maabara hii na kikubwa wanachojivunia ni kuweza kuchukua vipimo
vya wagonjwa hadi mlangoni kwao kwenye vijiji zaidi ya 45, wakati mgonjwa
halazimiki kutembea umbali mrefu na majibu anayapata hapohapo,” alisema.
“Kwa wastani maabara hii inaweza kuhudumia watu 150
kwa siku na kila kipimo kinachowekwa kinatumia muda wa sekunde mbili kupata
majibu yake. Taarifa zake zinaweza kuhamishika kwa kutumia USB au Bluetooth connection,” aliongeza.
Bw. Bhatnagar ambaye alikuwa miongoni mwa
wafanyabiashata 50 waliombatana na Waziri Mkuu wa India aliyezuru Tanzania Jumamosi
iliyopita, alisema maabara hiyo ina vifaa vyote muhimu kama Biochemistry
Analyzer, Centrifuge, Incubator, Data Recorder with Patient Data Management
Software, Micropipettes na
power back-up. Pia inakuwa na Laptop ndogo ya kupokelea na kuhifadhi taarifa
za vipimo vya wagonjwa.
Pia
alimweleza Waziri Mkuu kwamba vifaa vya maabara hiyo vinaweza kufanya kazi
kwenye mazingira yasiyohitaji ubaridi kwani vina uwezo wa kuhimili joto kuanzia
nyuzijoto 00 hadi nyuzijoto 500.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu ambaye alimwita Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya aje kushuhudia maabara
hiyo, alisema ameguswa baada ya kubaini kuwa maabara hiyo inaweza kufanya
vipimo vingi vikiwemo vya malaria, magonjwa ya ini, na moyo.
Kwa upande wake, Dkt. Ulisubisya alimweleza Bw. Bhatnagar kwamba itabidi maabara hiyo pamoja
na vifaa vyake ikafanyiwe uchunguzi juu ya matumizi na kwamba vikikamilika
atapatiwa ripoti kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA).
“Utatakiwa
kuandika write-up na kuiwasilisha TFDA na wakikamilisha uchunguzi, watatuletea
taarifa ambayo tutaituma kwako,” alisema.
Vilevile,
Dkt. Ulisubisya alimweleza Waziri Mkuu kwamba ameridhika na wastani wa gharama
za vipimo kwa kila mgonjwa ambayo ni kama sh. 15 lakini bei ya maabara hiyo iko
juu. Awali, alielezwa na Mkurugenzi Mtendaji huyo kuwa bei yake ni rupia za
India 326,000 (sawa na sh. milioni 10.4).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMATANO, JULAI 13, 2016
No comments:
Post a Comment