HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 01, 2016

GGM yachangia Milioni 400 kwa ajili ya Madawati 6,000 Geita

Naibu Waziri  wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mhe. Seleman Jafo alialikwa kuwa mgeni rasmi katika tukio la kuchangisha fedha kusaidia tatizo la uhaba wa madawati katika mkoa wa Geita.

Katika tukio hilo, Mkoa wa Geita ulifanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi za kitanzania Bilioni 1.7 ambazo zinaweza kutengeneza madawati takribani 23,200 kwa bei ya wastani wa Shilingi za Kitanzania 75,000. 

Kiwango cha madawati yaliyochangishwa kinapunguza tatizo la madawati mkoani Geita na kufikia asilimia 34 ya upungufu uliopo hivi sasa.

Katika tukio hilo, Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) pekee ulifanikiwa kuchangia Shilingi za Kitanzania 444,000,000.00 (Milioni mia nne arobaini na nne) ambazo ni sawa na mchango wa madawati 6000 ambayo ni asilimia 25 ya michango yote iliyotolewa katika tukio hilo la uchangiaji madawati mkoani Geita.

Akizungumzia mchango huo wa madawati, Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita Bw Terry Mulpeter amesema kuwa GGM inaendelea kujihusisha katika kuchangia elimu mkoani Geita kwa kuwa ndiyo fursa endelevu ya kuwakomboa wananchi na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Terry Mulpeter.
“Kwakutambua umuhimu wa elimu, GGM imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwenye ujenzi wa miundo mbinu ya elimu.

Mgodi umechangia zaidi ya Shilingi Bilioni 10 za kitanzania kujenga shule ya wasichana ya Nyankumbu Mkoani Geita ambapo zaidi ya wasichana 800 wanapata maarifa kwenye michepuo ya Sayansi” anaeleza Bw Mulpeter na kuongeza kuwa mchango wa GGM umefanikisha pia shule hiyo kuwa na Kompyuta za kutosha pamoja na vifaa vya kisasa katika maabara na mazingira ambayo ni rafiki kwa wanafunzi kujisomea pamoja na nyumba  bora kwa waalimu kuishi. Hayo yakiwa na lengo la kuweka mazingira bora ya elimu kwa mkoa wa Geita”

Bw Mulpeter amesisitiza kuwa elimu ni mojawapo ya haki muhimu za binadamu.“Ndugu zangu, elimu ni jambo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. GGM inaamini kuwa kuweka mazingira bora ya kusomea ili watoto wetu wengi wahitimu vyema elimu ya msingi na sekondari na kuendelea na masomo ya juu itakuwa chachu ya maendeleo la taifa letu”

Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita amemalizia kwa kusistiza kwamaba Mgodi wa GGM unaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika jitihada za kuleta wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Pages