HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 28, 2016

TACAIDS: UKIMWI BADO NI JANGA

TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) imesema licha ya kuwapo kwa  mafanikio mengi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa  Ukosefu wa Kinga mwilini(Ukimwi) lakini bado ugonjwa huo ni janga kubwa duniani.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume hiyo  Dk. Leornad Maboko alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mikakati ya kupunguza Ukimwi na mafanikio yake.
Alisema takwimu zinaonyesha maambukizi ya mapya ya Virusi vya Ukimwi(VVU)  yalikadiriwa kuwa watu mil 2.1 duniani kote, ambapo yameshuka kwa asilimia 50 miongoni mwa watoto duniani lakini kwa watu wazima hayajashuka tangu 2010.
Alisema kwa mwaka 2015 duniani walikuwa watu milioni 37 walioambukizwa VVU, ambapo Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika walikuwa milioni 17 huku Tanzania wakiwa milioni 1.4 ambayo ni sawa na asilimia 7 ya watu waishio na VVU Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
“Pamoja na baadhi ya mafanikio katika mapambano dhidi ya Ukimwi, lakini bado ni janga kubwa duniani, Afrika na nchini Tanzania. …Nchini Tanzania, bado kuna makundi na maeneo ambayo kiwango cha maambukizi ya VVU ni bado kipo zaidi ya wastani wa kitaifa,” alisema.
Dk. Maboko alisema, “tafsiri ya takwimu hizi ni kuwa tusibweteke na mafanikio yaliyopo hivyo mapambano dhidi ya VVU yawe endelevu, kama nchi tunatakiwa kuweka nguvu nyingi kifedha na kimkakati katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha VVU pamoja na kuendelea kuimarisha utafiti na ukusanyaji wa tafiti ili kuendelea kubaini na kupanga mipango dhidi ya VVU inayoongozwa na takwimu,”.
Alisema dunia imejiwekea lengo la utokomeza Ukimwi kama janga ifikapo 2030, ambapo ili kufikia lengo hilo, shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu mapambano dhidi ya Ukimwi(Unaids) limeweka malengo ya muda wa kati ya tisini tatu(90-90-90).
Aidha alisema mchakato wa kuchangia mfuko wa Ukimwi ambao ulizinduliwa na Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu ni endelevu hivyo ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuendelea kuchangia.
“Mfuko huu wa udhamini wa masuala ya Ukimwi una lengo la kuhakikisha uwepo wa rasilimali za kutosha na uhakika kutoka mapato ya ndani na kupunguza utegemezi kutoka kwa wahisani ambao wengi wameanza kujitoa,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages