Mkurugenzi wa NMB, Ineke Bussemaker (kushoto), akikabidhi moja kati ya kompyuta 50 zilizotolewa na benki ya NMB, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, kwa ajili ya Shule za Msingi na Sekondari visiwani Zanzibar. (Na Mpiga Picha Wetu).
Benki ya NMB imekabidhi msaada wa kompyuta 50 kwa Shule za Msingi na Sekondari visiwani Zanzibar kama njia ya kuunga Mkono juhudi za serikali kuboresha elimu.
Msaada huo utazinufaisha shule za msingi na sekondari tisa na chuo kimoja cha ualimu ambacho kitapata kompyuta mpakato tano.
Kompyuta hizo ni sehemu ya kompyuta zaidi ya 250 ambazo tayari zilishakabidhiwa kwa upande wa Tanzania bara kwaajili ya shule za msingi na sekondari.
Kompyuta hizi zilishatumika na benki ya NMB kwa miaka mitatu huku zikiwa bado kwenye hali nzuri kimatumizi na hivyo kuona haja ya kuzipeleka kwenye mashuleni hasa shule zenye umeme kwaajili ya somo la TEHAMA kwa vitendo.
Akikabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa NMB - Bi Ineke Bussemaker alisema benki ya NMB inaunga Mkono juhudi za serikali katika katika kukuza Kiwango cha elimu nchini hasa masomo ya TEHAMA.
“Tumetoa msaada wa kompyuta 50 kwa ajili ya shule za msingi na sekodari, kompyuta hizi zipo katika hali nzuri kwa matumizi ya wanafunzi na wataalamu wetu wa ICT wamethibitisha na tunaamini zitatumika vizuri na kuwa na faida katika masomo ya TEHAMA” Alisema Bi Bussemaker.
Bi Bussemaker aliongeza kuwa NMB imekuwa ikisaidia jamii katika hususani katika sekta ya afya na elimu na hivyo kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya Zanzibar kusaidia kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.
“Leo tunakabidhi kompyuta 50 ambazo zilishatumika ndani ya benki kwaajili ya shule za msingi na sekondari zenye umeme, chumba cha kompyuta na walimu wa Tehama.
Hii si mara ya kwanza kutoa msaada wa namna hii, tulifanya hivyo mwaka 2014 ambapo tulitoa kompyuta 10 kwaajili ya shule za Mwembeladu na Makadala zote za hapa Zanzibar.” Alisema Bi Bussemaker
Akipokea kompyuta hizo kwa niaba ya wanufaika, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali – Bi Riziki Pembe Juma alisema msaada huo umekuja muda muafaka ambapo serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imeweka nguvu kubwa katika kuhakikisha somo la Tehama linafundishwa mashuleni kwa vitendo na si kwa nadharia tena.
“Kama serikali tunawashukuru kwa msaada ambao mmetupatia, tumekuwa tukifanya jitihada za kutoa kompyuta kwa shule zetu lakini bado tuna na changamoto nyingi, kupitia msaada huu tutahakikisha zinakwenda katika shule ambazo tayari zimeunganishwa umeme ili zilete tija kwa walengwa,” alisema Mh Riziki
Kwa Mwaka 2017, NMB imetenga Zaidi ya shilingi bilioni 1 kwaajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu. Kwa mwaka 2016, zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 zilitumika kusaidia sekta ya afya na elimu ambapo kwa sekta ya elimu, zaidi ya shilingi Milioni 900 zilitumika kutengeneza madawati kwaajili ya shule za msingi na sekondari nchini. Kwa Zanzibar, zaidi ya madawati 450 yaligawiwa katika shule.
NMB ina matawi zaidi ya 180, ATM Zaidi ya 600 nchi nzima pamoja na idadi ya wateja inayofikia milioni mbili na laki tano Kiwango kinachoifanya benki hiyo kuwa kubwa kuliko zote hapa nchini.
No comments:
Post a Comment