HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 08, 2017

Rais Magufuli apokea hati za utambulisho za mabalozi 6

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akipokea hati za utambulisho toka kwa Balozi wa  Burundi  nchini Mhe. Gervais Abayeho Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatano Februari 8, 2017.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 08 Februari, 2017 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 6 kutoka nchi mbalimbali walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi wote wana makazi yao hapa Jijini Dar es Salaam na wamekabidhi hati zao za utambulisho kwa Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Mabalozi hao ni Balozi wa Ufalme wa Kiarabu wa Saudi Arabia Mhe. Mohamed Ben Mansour Al Malek, Balozi wa Ufalme wa Morocco Mhe. Abdelilah Benryane, Balozi wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Benson Keith Chali, Balozi wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Lucas Domingo Hernandez Polledo, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mhe. Mousa Farhang na Balozi wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Gervais Abayeho.

Pamoja na kupokea hati zao za utambulisho Mhe. Rais Magufuli amewakaribisha Mabalozi hao hapa nchini na kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi zao katika nyanja mbalimbali hasa uchumi kwa manufaa ya pande zote.

“Mhe. Balozi najua kuwa Saudi Arabia imekuwa ikishirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu na bado kuna miradi mingi tutashirikiana, naomba umfikishie salamu zangu nyingi Mhe. Mfalme wa Saudi Arabia kuwa tutaendelea kushirikiana” amesema Mhe. Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na Mhe. Balozi Mohamed Ben Mansour Al Malek.

“Nitafurahi sana kuona Cuba inakuja kujenga viwanda vingi vya kuzalisha dawa hapa Tanzania, tunataka kuondokana na uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi ili kupunguza gharama kubwa ambazo Serikali inabeba kwa sasa kwa kuagiza dawa kutoka nje” Mhe. Rais Magufuli amemueleza Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Lucas Domingo Hernandez Polledo.

Balozi wa Morocco hapa nchini Mhe. Abdelilah Benryane amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na mambo mengine ambayo nchi hiyo inaendelea kushirikiana na Tanzania tayari imeanza mchakato wa kutekeleza ahadi ya Mfalme wa Morocco Mtukufu Mohammed VI ya kujenga uwanja wa mpira Mjini Dodoma.

Akizungumza na Balozi wa Zambia hapa nchini Mhe. Benson Keith Chali Mhe. Rais Magufuli amesema anatarajia ujio wake pamoja na mambo mengine utasaidia kuharakisha mchakato wa kuimarisha utendaji kazi na ufanisi wa reli ya TAZARA na bomba la mafuta la TAZAMA kwa manufaa ya nchi hizi mbili.

Kwa Balozi wa Burundi hapa nchini Mhe. Gervais Abayeho, Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hiyo kama ndugu na marafiki wa kihistoria na kwamba anaamini kuwa juhudi zinazoendelea kufanywa na Mpatanishi wa Mgogoro wa kisiasa nchini humo Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu nchini Tanzania zitazaa matunda.

Mabalozi wote wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa hatua anazochukua kujenga uchumi wa Tanzania, kukabiliana na rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na kusimamia uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

08 Februari, 2017

No comments:

Post a Comment

Pages