HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 21, 2017

Timu ya Taifa mbio za Nyika hadharani

NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
 
SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limetangaza wanariadha waliofanikiwa kuchaguliwa kuunda timu ya Taifa ya Mbio za Nyika itakayoiwakilisha nchi katika Mashindano ya Dunia yatakayofanyika jijini Kampala Uganda, Machi 26 mwaka huu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini hapa jana, Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday, alisem wanashukuru kwa kukamilisha hatua ya kwanza na ya muhimu ya maandalizi ya kuelekea Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika ‘World Cross Country’ Kampala Uganda, baada ya kufanikiwa kupata timu ya Taifa.

“Kama mtakumbuka, Jumamosi, Februari 18 RT iliendesha Mashindano ya Taifa ya Mbio za Nyika katika Viwanja vya Gofu mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na kushirikisha mikoa zaidi ya 11 Tanzania Bara na Visiwani, ambapo wakongwe wengi wa riadha wamekiri kwamba mwamko waliouona juzi haujatokea tangu mwaka 1991 kwenye mashindano yaliyofanyika Arusha eneo la Mushono,” alisema Gidabuday na kuongeza.

Mwaka huo wa 1991, ndiyo mwaka ambao mtanzania pekee Andrew Sambu alishinda mashindano ya Junior ya Dunia Antwerp Belgium, kwa mfano huo sisi Shirikisho la Riadha Tanzania tuna imani kubwa na timu iliyochaguliwa mwaka huu, tunakwenda Uganda kifua mbele, hatuogopi chochote, mataifa mengine nayo yanafahamu kwamba watanzania wameamua safari hii.

Alisema mara baada ya mashindano hayo ya Taifa, Kamati ya Ufundi ya RT iliketi na kuwachagua wachezaji na makocha wafuatao kuunda timu ya Taifa tayari kwa mashindano hayo ya Dunia.

Wanaume Senior Kilomita 10 ni Emmanuel Giniki (Manyara), Basil John (CCP/Kilimanjaro), Gabriel Geay (JKT/Arusha), Fabian Joseph (Arusha), Wilbado Peter (CCP/Kilimanjaro), na Josephat Joshua (CCP/Kilimanjaro).

Kwa upande wa Wanawake Senior Kilomita 10, Gidabuday aliwataja Magdalena Shauri (JKT/Arusha), Angelina Tsere (JKT/Arusha), Failuna Abdi (Arusha), Sara Ramadhani (Arusha), Jackline Sakilu (JWTZ/Arusha), na Siata Kalinga (JWTZ/Arusha).

Kwa upande wa Wanaume Junior Kilomita 8 waliochaguliwa ni Francis Dambel (Manyara), Yohana Elisante (JKT/Arusha), Ramadhani Juma, Elisha Wema, Anthony Wema na Joshua Elisante (Wote kutoka Arusha).

Wanawake Junior Kilomita 6 waliopenya ni
Cecilia Ginoka, Maicelina Issa, Asha Salum (Wote JKT/Arusha), Noela Remy (Manyara), Elizabeth Boniface (Singida), na Amina Mgoo (JKT /Arusha).

Kwa upande wa Relay Wanaume inayoundwa na wachezaji wawili, Gidabuday aliwataja Faraja Damas wa JKT Arusha na Marco Sylvester kutoka Singida wakati kwa upande wa wanawake watatangazwa hivi karibuni kutokana na sababu za kiufundi.

Katibu huyo, aliwataja makocha waliopendekezwa kuwa ni Naasi Gwagwe wa CCP Moshi, Thomas Tlanka wa klabu ya Talent ya Arusha, Francis Nade kutoka Manyara, Zakaria Barie wa Arusha na Lwiza John kutoka Mbeya.

Alisema timu hiyo inatarajiwa kuingia kambini mara baada ya mashindano ya Kilimanjaro Marathon yatakayofanyika Februari 26 mwaka huu mjini Moshi, Kilimanjaro.

Aidha, aliwapongeza viongozi wakuu wa RT, Rais wa Shirikisho Anthony Mtaka kwa maono yake, bidii za kutafuta namna yoyote ya kuendeleza mchezo wa riadha na suala la kutoa zawadi kwa washindi katika mashindano ya mwaka huu ni wazo lake na ndiyo hali iliyoleta hamasa zaidi.

“Pia suala la kuendesha mashindano mikoani kikanda ni wazo lake, sisi wengine tuliweka ‘strategies’ ili ‘idea’ ile ikae kiufundi zaidi…Pia kwa uamuzi wake wa kipekee, kuamua kuwalipia ada ya ushiriki wa mbio za Kilimanjaro Marathon, wanariadha wote walioshiriki mbio za Nyika za Taifa kwa ‘categories’ zote na kushika nafasi kumi za juu,” alisema Gidabuday.

Aidha, aliwashukuru Makamu wa Kwanza wa Rais RT ambaye pia ni Mwenyekiti Kamati ya Fedha, William Kallaghe na Makamu wa Pili wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti Kamati ya Ufundi, Dk. Ahmad Ndee kwa kusimamia taratibu zote za kifedha, kiutawala na kiufundi sambamba wajumbe wote wa Kamati Tendaji na Kamati ya Ufundi wakishirikiana na Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro (KAA).

Pia alitoa pongezi za kipekee kwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Riadha Mkoa wa Singida, Miraji Mtaturu, kwa ushirikiano wake mkubwa katika maendeleo ya riadha, ikiwamo kujitolea kufanikisha mashindano ya wazi kwa mikoa ya kanda ya kati ya vijana, ambayo yatafanyika mwezi ujao maalumu kupata timu ya Taifa ya Vijana kwa ajili ya mashindano ya vijana ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ambako Tanzania itakuwa mwenyeji.

No comments:

Post a Comment

Pages