Na Marym Nassor, Pemba
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mmanga Mjengo Mjawiri, amewataka waalimu kuacha kusomesha kwa mazoea, na badala yake kubadilika ili kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi hapa nchini.
Alisema kuwa, Wizara pamoja na kueko maendeleo makubwa ya elimu, lakini iko haja zaidi yakuhakikisha maendeleo hayo yanaimarika siku hadi siku.
Naibu huyo aliyasema hayo wakati alipokua akizungumza na waalimu wa skuli 14 za Msingi Kisiwani Pemba, katika Skuli ya Maendeleo ya Ngwachani, alisema kazi hiyo itafanikiwa kufuatia waalimu kufanyakazi yao kwa kufuata sheria na kanuni za kazi zao.
“Tufanye kazi kwa juhudi zote, lazima mwalimu somo analolifundisha alimudu kwa mujibu wa kiwango chake cha elimu ndio aweze kufundisha darasani hii ni sifa muhimu kwa mwalimu bora” ,alisema.
Aidha alisema kuwa, hakuna maendeleo katika taifa lolote duniani, iwapo wananchi wake hawatokuwa na elimu yenye kiwango bora hivyo ni vyema kila mwalimu kubuni njia mbadala za ufundishaji katika darasa lake.
Nae Mwalimu wa Skuli ya Dodo Pujini Khalfan Khamis Ali alisema, Waalimu wamekua wakikumbana na changamoto ikiwemo kukosekana ushirikiano baina ya waalimu na Wazazi jambo ambalo limekua likiwawarejesha nyuma waalimu katika utendaji wao wa kazi.
“Utoro pia kwa wanafunzi hasa katika siku za Ijumaa umekua ni changamoto kwetu, na hali hii pia inachangiwa na wazazi kutokushirikiana na waalimu kujua taarifa za mwanafunzi”, alisema.
Kwa upande wake Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Mizingani Mkoani Mzee Ramadhan Othman alisema, ipo haja ya Serikali kurejesha Chuo Cha Ualimu Mkurumah ili waalimu wa waweze kufaidika zaidi na mafunzo ya Elimu ya Msingi inayotolewa.
Naibu waziri wa elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bado anaendelea na ziara yake ya kikazi ambapo hufanya mikutano na waalimu wa Skuli mbali mbali Kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment