Na Daudi Manongi-MAELEZO, DODOMA.
Waajiri wote nchini yakiwemo makampuni ya Madini wametakiwa kutekeleza matakwa ya Sheria ya kazi kwa lengo la kulinda haki za wafanyakazi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Ajira Kazi na watu wenye Ulemavu Mhe. Anthony Mavunde wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge leo Mjini Dodoma.
“Makampuni haya yana wajibu mkubwa wa kulinda haki za wafanyakazi,kupunguza migogoro isiyo ya lazima sehemu za kazi na kuongeza tija na uzalishaji mahala pa kazi.”Aliongeza Mhe.Mavunde.
Aidha amesema Ofisi yake imeendelea kutekeleza majukumu yake ya usimamizi wa Sheria kwa kufanya kaguzi sehemu za kazi kwa lengo la kuhakikisha kuwa waajiri wanazingatia matakwa ya Sheria,elimu ya Sheria za kazi inatolewa kwa waajiri,wafanyakazi na vyama vyao ili kuongeza uelewa wao katika kutekeleza Sheria.
Kuhusu ukaguzi wa mikataba kwa kampuni zinazofanya kazi migodini amesema Serikali iliunda kikosi ambacho kilishirikisha Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu,NSSF,SSRA,OSHA ,Mamlaka ya Mapato Tanzania na Wakala wa Ukaguzi wa Madini.
Amesema kikosi kazi hiki kilipewa jukumu la kufanya ukaguzi wa kina kwenye migodi iliyopo kanda ya ziwa na kaskazini kwa lengo la kuangalia hali halisi ya utekelezaji wa Sheria za kazi,afya na usalama mahali pa kazi,masuala ya hifadhi ya jamii,fedha na kodi.
Pamoja na hayo amesema kuwa Serikali inatambua umhimu wa uwekezaji katika kukuza fursa za ajira kwa watanzania na kuchangia kukua uchumi kwa ujumla.
“Serikali itaendelea kusimamia sheria za kazi ili kuhakikisha kuwa waajiri wote nchini wanatimiza wajibu wao na wawekezaji wamepata nafasi ya kuwekeza na kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu kwa kufuata sheria zilizoko nchini”Alisisitiza Mhe.Mavunde.
No comments:
Post a Comment