Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea Jumamosi Mei 6 na Jumapili Mei 7, mwaka huu kwa jumla ya michezo sita.
Kwa mujjibu wa ratiba, michezo ya Jumamosi kutakuwa na michezo mitano ilihali Jumapili kutakuwa na mechi moja.
Michezo ya Jumamosi itakuwa ni kati ya Toto African na JKT Ruvu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Majimaji ya Songea itakuwa mwenyeji wa Mwadui kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Kagera Sugar itaalikwa na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati Young Africans ya Dar es Salaam itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Siku hiyo ya Jumamosi Mei 6, mwaka huu Azam FC itaialika Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Mbagala, Dar es Salaam ilihali Jumapili kutakuwa na mchezo kati ya Simba SC na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
TFF, WILDAID WASAINI MAKUBALIANO KUPIGA VITA UJANGILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Taasisi ya kupigania uhai wa maisha ya wanyama wa mbugani ya Wildaid Alhamisi Mei 4, mwaka huu kwa pamoja wamesaini makubaliano ya vita dhidi ya ujangili.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwakilishi wa taasisi hiyo, Lily Massa.
Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Rais wa TFF Jamal Malinzi alisema kwamba, “Hii ni sehemu nyingine ya TFF kujihusisha na shughuli za kijamii licha ya kuwa na majukumu ya kusimamia maendeleo ya mpira wa miguu katika kukuza na kuendesha mashindano.”
Malinzi amesema TFF inaendeleza utamaduni wa shughuli mbalimbali za jamii kwani hata kwa Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Tenga enzi za utawala wake akiwa kiongozi mkuu wa mpira wa miguu, alifanya hivyo katika kampeni za kupinga maambukizi mapya ya UKIMWI.
“Wengi mtakumbuka kuwa kulikuwa pia na vita vya kupigania afya za watoto na kupigania uhai wao pia kampeni za amani ambazo mpira wa miguu umetumika kuelimisha,” amesema.
Kwa hatua hii ya sasa, Rais Malinzi amesema kwamba TFF, inaingia makubaliano hayo na kuiteua timu ya taifa ya vijana Tanzania maarufu kama Serengeti Boys kusimama kidete kupinga uwindaji haramu wa wanyama mbugani kwa kuwa ni hazina kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wa Mwakilishi wa WildAid, Lily Massa, alishukuru kuingia kwa makubalino hayo akisema kwamba ndoto zao za kupiga vita uwindaji haramu na ujangili, itafanikiwa.
“Tunashukuru kuingia programu hii na ninaamini Mungu atatusaidia,” amesema Massa ambaye taasisi yake iko karibu kila nchi yenye wanyama wa mbugani.
Katika hatua nyingine, Rais Malinzi aliitakia kila la kheri Serengeti Boys ambayo kwa sasa inajiandaa kuingia Gabon kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Mei 14, mwaka huu ambako Serengeti Boys ambayo iko Kundi B itakuwa Libreville - Mji Mkuu wa Gabon. Timu nyingine za Kundi B ni Mali, Niger na Angola.
ABDULRAHMAN MUSSA MCHEZAJI BORA WA VPL MWEZI APRILI, 2017
Mchezaji wa timu ya Ruvu Shooting FC, Abdulrahman Mussa amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Aprili kwa msimu wa 2016/2017.
Abdulrahman aliwashinda wachezaji Jafar Salum wa Mtibwa Sugar FC na Zahoro Pazi wa Mbeya City.
Katika mwezi wa Aprili kulikuwa na raundi tatu na timu ya Ruvu Shooting ilicheza michezo miwili ambayo Abdulrahman alicheza dakika zote 180 na kufunga magoli manne(4) kati ya matano yaliyofungwa na timu yake na hivyo kuifanya timu yake kufikia nafasi ya tisa(9) kutoka nafasi ya kumi(10) katika msimamo wa Ligi ya Vodacom.
Abdulrahman alifunga Hat Trick (magoli matatu) katika mchezo wa Ruvu Shooting dhidi ya Majimaji uliofanyika katika uwanja wa mabatini Mlandizi.
Kwa kushinda tuzo hiyo, Abdulrahman Mussa atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja (1,000,000/) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.
……..……………………………………………………………….………………………
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
No comments:
Post a Comment