HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 02, 2017

WAZIRI DKT. TIZEBA: “WEZESHENI WASINDIKAJI MAZIWA ILI KUONGEZA TIJA TASNIA YA MAZIWA”

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba (kushoto), akizungumza na maofisa wa Benki ya Kilimo juu ya umuhimu wa kuharakisha utoaji wa mikopo kwa wasindikaji wa maziwa nchini. (Na Mpiga Picha Wetu).

Na Mwandishi Wetu, Bukoba
Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles Tizeba ameiagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) kuharakisha kutoa mikopo kwa wasindikaji wa maziwa nchi ili kuongeza tija kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini.
Waziri Dkt. Tizeba alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa Benki hiyo katika Kilele cha Maadhimisho ya Kampeni ya Wiki ya Maziwa iliyokuwa ikifanyika Kitaifa mjini Bukoba, mkoani Kagera tangu tarehe 28 Mei na kufikia kilele chake tarehe 01 Juni, 2017.
Dkt. Tizeba alisema utoaji wa mikopo kwa wasindikaji una umuhimu wa kipekee kwa kuwa utachangia uhakika wa masoko kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini hali itakayochochea tija kwa wafugaji hao hivyo kuchagiza lengo la Serikali la Awamu ya Tano ya kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuweza kunufaika na sekta hizo.
“Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi hivyo uanzishwaji wa Benki ya Kilimo lazima usaidie katika kuhakikisha wasindikaji wa maziwa wanapata huduma za TADB kwa wakati ili tupate uhakika wa masoko kwa wafugaji wetu ili tuiinue Tasnia ya Maziwa ili ichangie ukuaji wa uchumi na maendeleo nchini,” alisema.
Kwa mujibu wa mpango kazi wa TADB, sekta ya mifugo ni mojawapo ya minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao na mifugo mbalimbali hasa katika uongezaji wa thamani wa ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa nchini. Na Benki imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa Ufugaji wa Ng’ombe wa Nyama na Maziwa ili kuongeza tija kwenye Tasnia za nyama na maziwa ili kuchagiza maendeleo katika tasnia hizo.
Katika kuhakikisha wasindikaji wa maziwa wananufaika na huduma za TADB, Benki hiyo inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka Kumi na Mitano (15)).
Kwa mujibu wa Mpango Kazi huo, mikopo hiyo ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka   kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

TADB ni taasisi ya serikali ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kutatua ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini ambao ulikuwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa; riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo; mikopo ya muda mfupi; masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo  na mazao ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

No comments:

Post a Comment

Pages