NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Fatma Rembo, ameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha benki maalum ya uwezeshaji wa wanawake na vijana ili kurahisisha upatikanaji wa mitaji, elimu ya biashara na huduma nyingine za kifedha kwa wananchi.
Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu wakati wa mkutano wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi uliofanyika Kalenga, mkoani Iringa, mbunge huyo alisema kuwa wanawake wengi, hususan wa vijijini, bado wanakabiliwa na changamoto ya kutofahamu mifuko mbalimbali ya uwezeshaji na masharti yake.
Alisema kuwa kuwepo kwa taasisi moja maalum ya kifedha kutasaidia kuongeza uwazi, ufanisi na urahisi wa upatikanaji wa huduma za mikopo kwa wanawake na vijana.
“Tunataka mwanamke wa Iringa asibaki kuwa mpokeaji wa mkopo mdogo tu, bali awe mfanyabiashara mkubwa, mzalishaji kamili na mshiriki kamili wa uchumi wa taifa,” alisema.
Katika hotuba yake, Rembo alimshukuru Waziri Mkuu kwa ziara zake za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini, akisema zimekuwa daraja muhimu kati ya wananchi na Serikali kwa kusikiliza kero na kutoa majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi.
Pia alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za afya na maendeleo ya wananchi, akitaja mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya mkoani Iringa.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina vituo vya afya 11, zahanati 81 pamoja na hospitali ya wilaya inayojengwa na ambayo imefikia hatua nzuri ya utekelezaji.
Mbunge huyo alieleza kuwa maboresho katika huduma za afya ya mama na mtoto yamechangia wanawake wengi kujifungulia katika mazingira salama na kupata huduma bora za afya.
Akizungumzia mikopo ya uwezeshaji, alisema zaidi ya Sh bilioni 3 zimetolewa kupitia vikundi mbalimbali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, hatua ambayo imewanufaisha maelfu ya wananchi na kusaidia kuboresha maisha yao.
Hata hivyo, alisema bado kuna haja ya kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wa kiuchumi ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na fursa zilizopo.
Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Iringa, Rembo alituma salamu za shukrani kwa Rais na kueleza kuwa wanawake wa mkoa huo wanaendelea kumuunga mkono na kumuombea katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuliongoza taifa.
Aidha, alimtakia Waziri Mkuu afya njema na mafanikio katika ziara zake za kutembelea wananchi na kusikiliza changamoto zao katika maeneo mbalimbali nchini.





No comments:
Post a Comment