*Asema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea mradi ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi II na kusema kwamba ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.
Amesema hayo leo (Jumamosi, Julai 08, 2017) alipotembelea mradi huo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia unaojengwa eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa mradi huo kutaliwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika, utakaowezesha kuendesha viwanda.
Amesema mkakati wa Serikali ni kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme ili Watanzania wapate umeme mwingi utakaosambazwa hadi vijijini kwa gharama nafuu.
“Tunataka tupate umeme wa kutosha ili viwanda vitakavyojengwa viwe na nishati ya uhakika na ya gharama nafuu. Ni wajibu wetu kuendelea kuimarisha utekelezaji wa miradi hii.” Amesema.
Naye, Meneja wa Mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi, Mhandisi Stephen Manda amesema gharama za mradi wa Kinyerezi II ni dola milioni 344.
Meneja huyo amesema tayari mradi huo umefikia asilimia 66.32 ya ujenzi wake na sasa wako katika hatua mbalimbali za kukamilisha, ikiwemo ujenzi wa misingi ya mitambo na jengo la kuendeshea mitambo.
“Pia tunaendelea na ujenzi wa nguzo za kupokelea laini ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Kinyerezi I hadi Kinyerezi II, ambapo mtambo wa kwanza wa megawati 30 utawashwa ifikapo Desemba 2017 na kila mwezi tutaingiza megawati 30 katika gridi ya Taifa.”
Amesema miradi iliyoko katika eneo hilo ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni Kinyerezi 1 (150MW), Kinyerezi I Extension (185MW ) na Kinyerezi II (240MW).
Mhandisi Manda ameongeza kuwa mradi wa Kinyerezi 1 (150MW) ulikamilika Machi 2015 na miradi mwili ya Kinyerezi 1-extension na Kinyerezi II inatarajiwa kukamilika mwaka 2018.
Mhandisi Manda amesema miradi mingine inayotarajiwa kujengwa katika eneo hilo ni wa Kinyerezi III (600 MW) na Kinyerezi IV utakaozalisha (450 MW).
Awali Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bi. Sophia Mjema ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda alisema mradi huo umewanufaisha wananchi wengi wa eneo hilo.
Alisema hadi sasa wananchi 100 wa eneo la Kinyerezi wameajiriwa katika miradi hiyo ambapo ni sawa na asilimia 40 ya watumishi wote.
Bi. Sophia alisema mbali na ajira pia wananchi wa eneo hilo watanufaika kwa kuboreshewa huduma mbalimbali za kijamii katika eneo hilo zikiwemo za maji na elimu ambapo wameahidiwa kupewa madawati ya shule tano.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 08, 2017
No comments:
Post a Comment