HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 08, 2021

TMDA YAAGIZA KUMBI ZA STAREHE KUTENGA SEHEMU ZA KUVUTIA TUMBAKU, SIGARA


Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bi. Gaudensia Simwanza  akitoa elimu kwa Wananchi waliofika kwenye banda hilo ndani ya banda lao Saba saba.

 

Na Andrew Chale, Saba Saba

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw. Adam Fimbo imesema katika majukumu ya kutoa elimu juu ya udhibiti wa Tumbaku ni pamoja na sehemu zenye mikusanyiko ya watu kutenga maeneo ya kuvutia tumbaku na wataoshindwa kufanya hivyo sheria itashika mkondo wake.

Akizungumza katika maonesho ya 45 ya Biashara Kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba) Mkurugenzi Mkuu huyo amebainisha kuwa, baada ya TMDA kukasimiwa udhibiti wa bidhaa za Tumbaku na mazao yake, imeanza kuandaa kanuni na  kutoa elimu zaidi kwa jamii.

Fimbo amesema kuwa hapo nyuma kulikuwa hakuna chombo cha kudhibiti Tumbaku na mazao yake hivyo Wizara imeikasimisha TMDA kufanya kazi hiyo ya udhibiti toka mwezi Aprili 2021.

"Kazi hii ni kuelimisha watu ili watumie bidhaa za tumbaku huku wakijua madhara yake na kufuata sheria hususan juu ya kutenga sehemu ya kuvutia sigara katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vile katika kumbi za starehe" amesema Fimbo.

Amesema kuwa madhara ya tumbaku ni mengi hivyo katika kulinda nguvu kazi lazima kuelimishwa juu ya madhara ya yatokanayo na na bidhaa hiyo ili mtumiaji afanye maamuzi sahihi baada ya kuwa na taarifa.

Mkurugenzi  huyo amesema kuwa watatoa elimu sehemu mbalimbali ikiwemo kupitia vyombo vya habari pamoja na kutumia fursa katika mikusanyiko mbalimbali ya watu.

Amesema mvutaji sigara akivuta na  akipuliza moshi wake madhara yake huwakuta wote ikiwa ni pamoja na yule aliyevuta hewa ya moshi huo.

"Wale ambao hawatafuata ni miongozo watachukuliwa hatua za kisheria zilizowekwa huku kukiwa na mikakati ya madhubiti ya kutoa elimu juu madhara ya tumbaku. Watu wenye umri chini ya miaka 18 kutojiingiza katika matumizi ya tumbaku. Kwa sasa TMDA imejikita katika kuandaa miongozo na  kutoa elimu juu ya Madhara yatokanayo na matumizi ya tumbaku. Madhara yanayoweza kutokea ni pamoja na ugonjwa wa kansa ya damu na mapafu" Alisema.

Na kuongeza kuwa, Maeneo mengi hayatengi sehemu za kuvutia sigara wakati anayevuta akipuliza moshi na ule moshi kumfikia mwingine basi huleta madhara  kwa asiyevuta pia"  Alimalzia Mkurugenzi Mkuu huyo wa TMDA.

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma, wa TMDA, Bi. Gaudensia Simwanza amesema TMDA inaendelea kutoa elimu kwa Umma kwenye banda lao lililopo ndani ya ukumbi wa Kilimanjaro.

"TMDA pia tunatoa elimu ya udhibiti wa bidhaa za dawa, vifaa tiba, vitendanishi na tumbaku kwa Wananchi wanaofika kwenye banda letu la sabasaba.

Ifahamike ni kosa kisheria kutafuna, kunusa na kuweka mdomoni bidhaa za tumbaku kama vile ugoro.

Pia kufahamu zaidi elimu ya udhibiti watu wanaweza kupiga simu bila malipo : 0800110084 au mitandao yetu ya Kijamii ya facebook, Instagram na Twitter @tmda ". Alimalizia Gaudensia Simwanza.

No comments:

Post a Comment

Pages