Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen
amemuagiza afisa afya wa wilaya ya Kalambo kuhakikisha anakagua usafi wa vyoo
na maeneo yanayo zunguka nyumba kwa wilaya nzima ili kujiepusha na ugonjwa wa
Kipindupindu katika Wilaya hiyo.
Ametoa agizo hilo katika mkutano na wananchi siku ya usafi
wa mwisho wa mwezi maarufu kama “Magufuli Day” baada ya Mkuu huyo kukagua
nyumba 12, maduka ya wafanyabiashara pamoja na soko katika makao makuu ya
wilaya hiyo huku nia ikiwa ni kutaka kujua hali ilivyo wanakojisaidia, wanakohifadhi
taka pamoja na hali ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
Katika ukaguzi huo amebaini kuwa wananchi wengi husafisha nje
ya nyumba tu huku nyuma ya majumba yao hali ikiwa mbaya jambo ambalo hupelekea
kuibuka kwa kipindupindu na kuisababishia serikali kuwa katika wakati mgumu kwa
magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika endapo usafi utazingatiwa.
“Leo nilipenda nione usafi wa matai, nimeuona na nimetoa “marks”
60, Nimepita karibu maeneo mbali mbali, usafi mnaoufanya ni wakuficha uchadu
kidogo, huku mbele kusafi lakini nyuma kuchafu sana, nawaomba hilo mlirekebishe”
Alisema.
Pia aliishauri halmashauri hiyo ya kalambo kuweza kusimamia sharia
za usafi zilizopo bila ya huruma ili kuleta mabadiliko na kuitaka halmashauri hiyo
kutenga fedha za makusanyo ya ushuru ili kuweza kuboresha hali ya usafi katika
mji huo.
Mwezi mmoja uliopita Wilaya hiyo ilikumbwa na ugonjwa wa
kipindupindu na kuua mtu mmoja na kuwaacha wengine ishirini katika hali mbaya
jambo ambalo serikali haitaki ijirudie.
“Juzi hapa kulitokea kipindupindu kule Kijiji cha Samazi,
hapana hatutaki watu wafe kwa kipindupindu, sasa nimeona choo kinamwaga maji
machafu kinyesi kinatoka nje bata wanapokea wanakula, hatupo salama,”
Alimalizia.
Pamoja na hayo Mh. Zelote alisisita kuwa usafi ni wa kila
siku si lazima kusubiri jumamosi ya mwisho wa mwezi na kueleza kuwa siku hiyo
imewekwa maalum ili kuwakumbusha wananchi kuwa wanahitajika kufanya usafi maeneo
wanayofanyia biashara pia na kuwa usafi ni muhimu.
No comments:
Post a Comment