Na
Ismail Ngayonga
MAELEZO
KILIMO
ndiyo Msingi wa Uchumi wa Taifa letu ambapo takribani asilimia 70 ya Watanzania
hutegemea sekta hiyo kama shughuli kuu ya Kiuchumi.
Hata hivyo,
pamoja na ukweli kwamba Nchi yetu ina eneo kubwa linalofaa kwa Kilimo takriban
Hekta Milioni 29.4, ni Hekta 290,000 tu, sawa na Asilimia Moja (1%)
zinazotumika kwa Kilimo cha Umwagiliaji Maji.
Kwa maana hiyo, Kilimo cha Umwagiliaji kinayo nafasi
kubwa ya kuwezesha kufikia Mapinduzi ya Kijani kwa kuwa kinatuhakikishia
uzalishaji endelevu wa mazao badala ya kutegemea mvua ambazo hazina uhakika wa
kiasi na wakati wa kunyesha katika msimu.
Serikali imekusudia kuongeza eneo la
umwagiliaji kufikia hekta 1,000,000 katika skimu za wakulima wadogo, wa kati na
wakubwa ifikapo mwaka 2020, ikiwa ni njia mojawapo ya kuongeza uzalishaji wa
Mazao ya chakula na biashara na kuongeza tija katika kilimo.
Akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya mapato na
matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson
Lwenge anasema hadi mwezi Machi 2017,
eneo linalomwagiliwa limeongezeka kutoka hekta 461,326 kwa mwaka 2015/2016 na
kufikia hekta 468,338.
“Eneo hilo linachangia asilimia 24 ya mahitaji
yote ya chakula nchini kwa sasa, ambapo hekta milioni 2.3 zina uwezekano
mkubwa, hekta milioni 4.8 zina uwezekano wa kati na hekta milioni 22.3 zina
uwezekano mdogo” anasema Mhandisi Lwenge.
Mhandisi Lwenge anasema katika mwaka
20176/18, Serikali inatarajia kutekeleza Mpango wa miaka 5 wa Programu ndogo ya
Umwagiliaji iliyolenga katika kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika skimu na
mabwawa ya umwagiliaji.
Waziri Lwenge anasema katika awamu hiyo,
Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika skimu 176, ukarabati
wa skimu 205, ukarabati wa mabwawa 30 na kujenga mabwawa mapya 40 ili kuvuna
maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na matumizi mengine kwenye
maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Mhandisi Lwenge anasema
Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wakulima na wataalam kuhusu usimamizi na
uendeshaji wa miundombinu ya umwagiliaji na kusajili vyama vipya 100 vya
wamwagiliaji katika skimu za wakulima wadogo; na kuimarisha vyama 442 vya
umwagiliaji vilivyopo.
Aidha Mhandisi Lwenge anasema Serikali
imeendelea kusimamia utekelezaji wa mradi wa kuendeleza skimu za umwagiliaji za
wakulima wadogo kwa awamu tatu katika Halmashauri 68 nchini.
Anasema kuwa hadi kufikia mwezi Machi 2017,
ukarabati na ujenzi wa skimu 45 za awamu ya kwanza umekamilika na utekelezaji
wa awamu ya pili ya mradi unahusisha ujenzi na ukarabati wa skimu 63 ambapo
ukarabati na ujenzi wa skimu 43 unaendelea; na taratibu za kuwapata Wakandarasi
wa skimu 20 zilizobaki zinaendelea katika Halmashauri husika.
“Katika mwaka 2016/2017, Wizara kwa
kushirikiana na Halmashauri za Wilaya 32 imeendelea kusimamia ukarabati na
uboreshaji wa skimu 45 za umwagiliaji za awamu ya kwanza zenye jumla ya hekta
13,722 na hivyo kumeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 461,326 hadi kufikia
hekta 468,338” anasema Waziri Lwenge.
Serikali inaendelea kupitia Mpango Kabambe wa
Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kubaini maeneo yanayofaa kwa kilimo cha
umwagiliaji, ambapo kazi hiyo inatarajia kukamilika katika mwaka 2018/2019.
Kukamilika kwa Mpango huo kutasaidia kuleta Mapinduzi ya Kijani nchini
ambayo yanahitaji matumizi ya utaalamu, mbegu bora, mbolea, madawa, zana bora
za kilimo pamoja na kuongeza eneo la Kilimo cha Umwagiliaji.
Aidha Mpango huo umekusudia kuweka mazingira mazuri ya kuongeza
Uzalishaji katika Kilimo; kuongeza Pato la Mkulima; kupunguza Umaskini Vijijini
na kushirikisha Sekta Binafsi kuleta uhakika wa Chakula katika Kaya.
No comments:
Post a Comment