WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watu wote wenye nia ya
kutaka kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini Tanzania kuhakikisha wanafuata
sheria, kanuni na taratibu.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 29, 2017) wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais (Uendelezaji Bishara) wa
kampuni ya PIRIOU, Bw. Michel Perrin.
Waziri Mkuu amekutana na Bw. Perrin jijini Paris nchini Ufaransa
kupitia ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa. Kampuni ya PIRIOU inataka
kuja nchini kuwekeza katika utengenezaji na ukarabati wa meli.
Akizungumza na muwekezaji huyo Waziri Mkuu alimshukuru kwa nia
yake ya kutaka kuwekeza nchini, ambapo alimtaka afuate sheria, kanuni na
taratibu za uwekezaji nchini.
“Tanzania ni sehemu nzuri ya uwekezaji kwa sababu kuna fursa
nyingi. Pia ni nchi yenye amani na utulivu wa kisiasa pamoja na mazingira
mazuri ya uwekezaji hivyo nakukaribisha sana.”
Kwa upande wake Bw. Perrin amesema ameamua kuja kuwekeza
nchini kwa kuwa Tanzania ni nchi salama na kwamba anauhakika wa kupata soko
ndani ya nchi pamoja na mataifa jiraji.
Amesema anaamini uwekezaji wake nchini Tanzania utakuwa na tija,
hivyo ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali na pia
atahakikisha anafuata sheria zote za nchi.
Pia Bw. Perrin alitumia fursa hiyo kumshukuru Balozi wa Tanzania
nchini Ufaransa, Balozi Samwel Shelukindo kutokana na ushirikiano anaompa
kuhusu masuala ya uwekezaji nchini.
Naye Balozi Shelukindo amesema atahakikisha anaendelea kutafuta
wafanyabiashara mbalimbali na kuwashawishi waje kuwekeza katika sekta
mbalimbali nchini
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, AGOSTI 29, 2017.
No comments:
Post a Comment