Jonas
Kamaleki- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ameamuru wateule wake wote waliotajwa kuhusika
na suala la upotevu wa madini ya Almasi na Tanzanite kukaa pembeni ili vyombo
vya usalama vifanye kazi yake.
Mhe. Rais ameyasema hayo leo
Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea ripoti za Kamati za Bunge
zilizochunguza madini ya Almasi na Tanzanite.
Amesema viongozi hao waliotajwa
iwe ni Waziri, Katibu Mkuu, Katibu Tawala, Mkurugenzi au kiongozi yeyote aache
kazi kwani Tanzania haiwezi kuendelea kuibiwa wakati viongozi hao wanaendelea
kuwa serikalini.
Rais Magufuli amesema mapendekezo
na yote yaliyoandikwa kwenye ripoti hizo mbili Serikali itayatekeleza kwa
asilimia 100.
“Nchi yetu ni ya maajabu kweli,
ajabu kubwa mojawapo ni kuwa hata hatujali raslimali zetu,”alisema Rais
Magufuli.
Akionyesha kusikitishwa na upotevu
wa raslimali hizo, Rais Magufuli amasema kuwa Tanzania imechezewa kwa kipindi
kirefu na kuwafanya watanzania kuishi maisha magumu wakati wanaoibia nchi
wakineemeka.
“Hao wanaotuchezea wanatuona sisi
si binadamu au ni majitu tu, wangetuona kama binadamu wangetupa basi asilimia
inayofaa,”alisema Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewataka
watanzania kuwa wazalendo kwa kujali na kuthamini mali na raslimali za umma ili
kuondoa nchi katika utegemezi wakati nchi ina kila kitu cha kuifanya kuwa
tajiri hadi kutoa misaada kwa nchi nyingine.
Ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama
kufuatilia mapendekezo na matokeo ya ripoti hizo kwa haraka ili hatua stahiki
ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Katika kusisitiza utekelezaji wa
hatua hizo, Rais Magufuli amekabidhi ripoti hizo mbili kwa Mkurugenzi wa TAKUKURU,
Bwana Valentino Mlowola na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venus Mabeyo.
No comments:
Post a Comment