Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe amewapongeza Wajasiriamali wa Tanzania kwa ushiriki wao
katika Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST.
Dkt. Mwakyembe ametoa pongezi hizo leo mjini Kampala nchini
Uganda katika viwanja vya Mashujaa Kololo alipotembelea kujionea namna tamasha
hilo lilivyopokelewa na wadau wake walioiwakilisha Tanzania wakiwemo
wajasiriamali toka vikundi mbalimbali, vikundi vya ngoma, vikundi vya sanaa ya
maigizo pamoja na baadhi ya wasanii.
Katika tamasha hilo, Dkt. Mwakyembe pia alipata fursa ya
kutembelea baadhi ya mabanda ya wajasiriamali hao pamoja na kuongea nao huku
akijionea bidhaa mbalimbali zinazouzwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki jambo ambalo limemfurahisha sana hususani kwa upande wa watu kutoka
Tanzania kwakuwa wamejaza mabanda yao kwa bidhaa kadha wa kadha.
“Tamasha hili linaonyesha utajiri mkubwa wa sanaa, utamaduni
pamoja na bidhaa tulizonazo kama nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
na hapa tumekutana kwasababu tunabadilishana mawazo na kuonyeshana bidhaa
mbalimbali za nchi zetu”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha, katika ziara hiyo, Dkt. Mwakyembe amewatoa wasiwasi
wajasiriamali hao kuhusu suala la upatikanaji wa masoko huku akiwaahidi kuwatafutia
fursa ya kuwapeleka wajasiriamali hao pamoja na bidhaa zao Bungeni mjini Dodoma
ili ziweze kupata soko kwa urahisi kupitia wabunge.
“Niwatoe wasiwasi wajasiriamali wote wa Tanzania mliohudhuria
hapa, nitahakikisha kuwa pindi tunaporudi nyumbani nitatafuta wasaa wa
kulishawishi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili nyie mpate nafasi ya
kuleta bidhaa zenu katika viwanja vya Bunge ili basi Wabunge wapate kujua haswa
vitu vizuri mlivyonavyo nah ii itawasaidia kuviuza kwa urahisi zaidi na
kujipatia vipato vyenu”, aliongeza Dkt. Mwakyembe.
Sambamba na hilo, Dkt, Mwakyembe amewahakikishia
wajasiriamali hao kuhusu suala la kujitangaza kupitia vyombo vya habari akisema
kwamba, atajitahidi kutoa ushawishi kwa vyombo vya habari nchini ili viweze
kuwapatia muda wa kuwatangaza wajasiriamali hao ili wapate kujulikana ikiwemo
shughuli wazifanyazo.
“Nitahakikisha kuwa siku mnapopewa nafasi ya kuja viwanja vya
Bunge basi mnapata muda wa kutosha katika vyombo vya habari ili mpate
kujulikana, hivyo kila mmoja wenu naamini atapewa nafasi ya kufanya mahojiano
kwa kujieleza shughuli azifanyazo na mahali anapopatikana na hii itawasaidia
kupata masoko zaidi toka kwa watu mbalimbali”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wao wajasiriamali hao wameshukuru Waziri Mwakyembe
kwa juhudi alizowafanyia hususani za kuhakikisha kwamba wanahudhuria kwa
kiwango kikubwa katika tamasha hilo, lakini pia ahadi aliyowapa ya kuwapeleka
Bungeni ili wakatangaze bidhaa zao na kuwatangaza katika vyombo vya habari
nchini.
Tamasha la JAMAFEST lilianzishwa mwaka 2013 nchini Rwanda na
baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kwa mwaka huu tamasha
hilo linafanyika mjini Kampala nchini Uganda ambapo pia tamasha hili
linatarajiwa kufanyika tena katika moja ya nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) mwaka 2019.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto)
akimsikiliza mjasiriamali wa Tanzania kuhusu baadhi ya bidhaa zilizopo katika banda lao wakati wa Tamasha la
Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika mjini
Kampala, Uganda 13 Septemba, 2017.
PICHA NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.
No comments:
Post a Comment