Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma
Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa kujenga
mitambo ya FM nchini kuimarisha usikivu maeneo mbalimbali ili wananchi waweze
kupata matangazo kutoka redio yao ya Taifa (TBC).
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Kyerwa
Innocent Sebba Bilakwate kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, lililohoji ni lini Serikali itawapatia
Wananchi wa Kyerwa haki yao ya kusikiliza Redio TBC ili kujua yanayoendelea
katika nchi yao kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya kubadilisha teknolojia ya
habari badala ya sasa kusikiliza Redio Rwanda na Uganda.
Mpango huo unatekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambao umeanza kutekelezwa katika wilaya
za Kibondo, Nyasa, Longido, Tarime pamoja na Rombo na utaendelea katika wilaya
nyingine ikiwemo Kyerwa kadiri bajeti inavyoendelea kuimarika.
“Kwa sasa kama ilivyobainishwa katika Hotuba ya
Bajeti ya Wizara ya mwaka 2017/2018, Serikali inaendelea kubadilisha mfumo wa
urushaji matangazo kupitia satelaiti uweze kuwa wa kisasa ili kuboresha usikivu
wa radio ya Taifa TBC hatua itakayosaidia wananchi kuendelea kupata habari
kupitia viongozi wao” amesema Naibu Waziri Wambura.
Naibu Waziri Wambura amebainisha kuwa zipo wilaya
84 nchini ambazo usikivu wa TBC umeshuka na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa
matangazo ya redio kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa baadhi ya
miundombinu ya radio, uwepo wa milima na uharibifu wa vifaa kutokana na radi
wakati wa mvua.
Aidha, Naibu Waziri Wambura amewataka Wabunge na
wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa endapo kutatokea
uharibifu wa vifaa vya kusaidia upatikanaji na usikivu wa matangazo ya radio ya
taifa TBC katika maeneo yao ili yaweze kufanyiwa marekebisho mapema na wananchi
waendelee kupata habari mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa.
Wilaya ya Kyerwa iko katika Mkoa wa Kagera ambapo
matangazo ya Redio yanapatikana kupitia mtambo wa TBC ulioko katika Manispaa ya
Bukoba ambao unasafirisha mawimbi ya Redio katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura akijibu
swali la Mbunge wa Kyerwa
Innocent Sebba Bilakwate leo Bugeni Mjini Dodoma lililohoji ni lini Serikali itawapatia Wananchi wa
Kyerwa haki yao ya kusikiliza Redio TBC ili kujua yanayoendelea katika nchi yao
kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya kubadilisha teknolojia ya habari badala ya
sasa kusikiliza Redio Rwanda na Uganda.
(Picha na Frank Mvungi, MAELEZO, Dodoma)
No comments:
Post a Comment