WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa
maji safi na salama pamoja na huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini zikiwemo
wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma.
Amesema Serikali
kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, itahakikisha wananchi
katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali
usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Waziri Mkuu
aliyasema hayo jana (Jumatano, Septemba 20, 2017) alipozungumza kwa nyakati
tofauti na wananchi wa wilaya ya Chemba na Kondoa waliomsimamisha katika maeneo
ya Chemba, Kalema, Bicha na Bereko akiwa njianu kuelekea mkoani Arusha kwa
shughuli za kikazi.
Alisema kwa
sasa Serikali imeendelea na uchumbaji wa visima virefu, vifupi pamoja na kuweka
mtandao wa mabomba ya kusamba maji katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na
ya wilaya hizo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo karibu na makazi
yao.
Pia Waziri Mkuu alisema wananchi wanatakiwa wazingatie sheria
ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye
maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Kufuatia hali
hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wawachukulie hatua watu wote watakaokutwa
wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji
wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.
Akizungumzia
kuhusu upatikanaji wa nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema hakuna kijiji
nchini kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa huduma hiyo katika awamu ya tatu ya
Mradi wa Nishati Vijijini (REA).
Ameagiza wakandarasi wamalize maeneo yaliyosalia katika
REA awamu ya pili ndipo waendelee na awamu ya tatu. Alisema Serikali imetenga
sh. trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000 ambavyo bado
havijaunganishiwa nishati hiyo.
“Rais wetu Dkt. John Magufuli anajali sana wananchi wake,
hivyo ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote
vikiwemo na vya wilaya za Chemba na Kondoa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo
ni sh. 27,000 tu.”
Pia Waziri Mkuu alisema
mwananchi hawatowajibika tena katika kulipia nguzo wala fomu za maombi
ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na
Serikali.
Waziri Mkuu
aliongeza kwamba lengo la Serikali ni
kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na kwa vile ambavyo viko kwenye
maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola, jambo ambalo litafungua fursa za
ajira na kukuza uchumi.
Awali mbunge wa
Chemba, Bw. Juma Nkamia, Mbunge wa Kondoa Mjini Bw. Edwin Sanda na Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji ambaye ni Mbunge wa Kondoa Vijijini
waliomba Serikali iwasaidie katika kutatua kero ya maji na umeme.
Walisema katika
maeneo mbalimbali ya majimbo yao wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa
huduma ya umeme pamoja na maji safi na salama hivyo kusababisha wananchi
kushindwa kushiriki vema kwenye shughuli za kimaendeleo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, SEPTEMBA 21, 2017.
No comments:
Post a Comment