Na
Thobias Robert
Kampuni ya Azam media kupitia Channel
(Idhaa) ya Sinema Zetu imeandaa Tamasha la Kimataita la Filamu hapa nchini kwa
lengo la kukuza, kuthamini kazi za Wasanii na maslahi yao pamoja na kukuza
lugha adhimu ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar
es Salaam na Mratibu wa Tamasha hilo Bi. Zamaradi Nzowa alipokuwa akizungumza
na Waandishi wa habari juu ya uzinduzi wa Tamasha hilo ambalo litahusisha Nchi za
Afrika, hususani nchi za Afrika Mashariki ambazo hutumia Lugha ya Kiswahili
katika kuandaa na kuigiza filamu zao.
Bi. Nzowa alieleza kuwa Idhaa ya
Sinema zetu imekuja na ujio huo mpya rasmi kwa mwaka 2017/2018 ambapo katika ujio huu
ameeleza kuwa wamekuja na Tamasha la Sinema Zetu International Film Festival
award, kwa lengo la kutoa tuzo kwaajili ya filamu zinazotumia lugha ya
Kiswahili na pia kuweka mchango katika
filamu za nchi yetu.
“Lengo kubwa la tamasha hili ni
kutoa wigo mpana kwa Tasnia ya Bongo Movies (uigizaji) kwa maana ya kwamba kama
channel kwa jinsi ilivyo inarusha tamthilia na sinema za Kiswahili za hapa
Tanzania kwahiyo tumekaa tukaona kwamba kwa sasa tuanze kuwapa tuzo na katika
safari yetu ya kuwapa tuzo pamoja na kufanya Tamasha,” alifafanua Bi.Nzowa.
Aidha aliongeza kuwa, Tamasha
hilo linalotarajia kufanyika kuanzia January Mosi mwakani, litaanza katika
mchakato wa kukusanya Sinema na Tamthilia kutoka kwa waigizaji wa mikoa ya
Tanzania bara na Zanzibar pamoja na nje ya nchi kuanzia sasa hadi
tarehe 30 Novemba mwaka huu, ambapo mwezi Desemba wataanza rasmi kuchuja filamu
kwaajili ya kupata filamu zitakazoingia katika kinyang’anyiro cha tuzo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu
wa Tamasha hilo Bw. Jacob Joseph alisema
kuwa, wanatarajia kushirikiana na wadau wa tamasha hilo kutoka mikoani kwaajili
ya kwenda kuonana na wadau wa filamu pamoja na kutoa elimu na kujenga uelewa
juu ya tamasha hilo pamoja na kukusanya
kazi zao.
“Hakutakuwa na upendeleo wa
aina yoyote katika tamasha hili ndio maana tutakwenda mikoani kukusanya kazi za wasanii wa mikoani
kwani tutakuwa hatujawatendea haki kama hatutoweza kuwafikia kwahiyo
tutawafikia wakazi wa mikoani katika mikoa 11 hapa Tanzania,” alisistiza Bw.
Joseph.
Aliongeza kuwa, Tamasha hilo
linahusisha tuzo za aina tano ambazo ni Filamu inayoanzia saa moja na
kuendelea, Tuzo za filamu fupi (Short film), Makala zenye dakika tano hadi
kumi, Tuzo maalumu ya makala inayozungumzia utaifa, mshindi katika Makala maalum atapewa cheti na zawadi
pamoja na tuzo ya mtu binafsi kama vile Muigizaji bora, Muongozaji bora, Mpiga
picha bora Muigizaji bora wa kike na kiume n.k.
Balozi wa Tamasha hilo ambaye
pia ni Muigizaji wa Bongo Movie Elizabeth Michael ‘Lulu’ ameeleza kuwa Tamasha
hilo ni mkombozi wa filamu hapa nchini kwani litawafanya wasanii waamke na
kutayarisha kazi zenye ubora kwa manufaa
yao, kukuza kipato, pia litaongeza ushindani kwa waigizaji na kukuza Lugha
adhimu ya Kiswahili.
“Pengine tupo wasanii wazuri,
wapo Waongozaji wazuri, wapo wapiga picha wazuri, lakini hapakuwa na kitu cha
kutupima hivyo kupitia tamasha hili tasnia yetu itaheshimika kujulikana na
kusonga mbele hivyo kwetu ni jambo zuri sana” alifafanua Lulu.
Aliongeza kuwa hakuna mafanikio
bila kipimo hata katika maisha mitihani ndiyo inamfanya mtu asonge mbele hivyo
ujio wa Tamasha na tuzo hizi ni faraja kwani ni Tuzo zilizokuwepo hazikuwa na
uwazi, usawa na wakati mwingine zilitolewa
kwa kujuana, tuzo hizi zitasidia kila mmoja kufanya kazi ya uhakikia
kwaajili ya ushindani kwani hazitakuwa na upendeleo wala kubebana.
Naye Prof. Martin Mhando ambaye
atakuwa Msimazi wa Majaji wa tamsha hilo ameeleza kuwa hakutakuwa na upendeleo
kwa mtu yeyote na kwamba ubunifu na utayarishaji bora ndiyo msingi wa tamthilia
kushinda tuzo hiyo.
Tutakuwa na kituo cha kupokea
Tamthilia kutoka katika mikoa, hili ni jambo jipya tumekuwa na tamasha la ZIFF
kwa mikoa 10 sasa lakini tumekuwa hatupokei kazi za watu kutoka mikoani hivyo
tumekuwa tukiwanyima fursa watu wa mikoani,” alisema Prof. Mhando.
Tamasha la kimataifa la sinema
zetu litafayika kwa mara ya kwanza hapa nchini na kilele chake kitakuwa 28
mwezi Februri 2018 ambalo litahusisha Visiwa vya Zanzibar, Miji ya Nairobi,
Tanga, Arusha, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Mtwara, Morogoro, Kigali, Bujumbura, Nairobi,
Kampala pamoja na Goma.
No comments:
Post a Comment