HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 21, 2017

Kampuni ya Tigo kushirikiana na Visions Sports wazindua mbio za Nyika Dodoma

Katika jitihada za kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano chini ya rais Dkt John Pombe Magufuli za kuimarisha afya kupitia michezo, Tigo Tanzania kwa kushirikiana na Visions Sports wamezindua mbio za nyika zitakazokuwa zikifanyika kila mwaka zikijulikana kama Dodoma Marathon.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari wakati wa Uzinduzi wa mbio hizo mkuu wa mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana amesema ujio wa mbio hizo kwa mkoa wa Dodoma ni fursa kubwa kwa wakazi wa makao makuu huku akiwapongeza Vision Sport na Tigo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano.

Amesema atazungumza na Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai ili kuwaalika wabunge kushiriki katika mbio hizo za Dodoma Marathon bila kuwasahau waandishi wa habari mkoani hapa kupitia club ya Central Press Club ( CPC ) na kwamba atazungumza na viongozi wa Chama cha Waandishi wa habari, tiGo Tanzania na Vision Spotrs ili kupata njia bora ya kuwasaidia Waandishi katika suala la michezo.

Akionyesha kuguswa na ujio wa Dodoma Marathon, Rugimbana amesema kilio chake kimekwisha kwani kwa siku nyingi amekuwa akipambana kuleta marathon Dodoma na hatimae Vision Sports na Tigo wametatua tatizo hilo na kwamba kutakuwa kamati ndogo ya mashindano itakayoongozwa na Mbunge wa jimbo la Dodoma mjini Antony Mavunde huku Katibu wa Chama cha Riadha  Mkoa wa Dodoma, Robert Mabonye akisema angetamani Dodoma marathon iende mbali zaidi hadi ngazi ya Kimataifa.

Mkurugenzi wa Vision Sports Ally Nchahanga amesema mbio hizo zitahusisha mbio ndefu za 42km, 21km,10km na matembezi ya 5km huku akiwashuru tigo kwa kudhamini Dodoma Marathon
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa tigo kanda ya Kaskazini Henry Kinabo amesema wanajivunia kudhamini tukio hilo litalowapa hamasa watu kuwa timamu kimwili na wenye afya ili watumie ujuzi wao wa kimichezo kung'ara.
Amesema tigo wanatazamia karibu na tukio hilo ili kuleta maendeleo na kuitambulisha Dodoma katika jumuiya ya kimaraifa.

No comments:

Post a Comment

Pages