HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 24, 2017

KOCHA MSWEDEN ALIPA TANO SOKA LA WANAWAKE

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya soka ya Wanawake ya Sweden, Pia Sundhage, akitoa maelekezo kwa wachezaji wa timu ya JKT Queen wakati wa Clinic ya mafunzo kwa makocha wa vituo vya michezo. 

NA MAKUBURI ALLY

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya soka ya Wanawake ya Sweden, Pia Sundhage amesema kwamba kwa mipango iliyojiwekea Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA) soka hilo hapa nchini litapiga hatua zaidi kimataifa.

Akizungumza katika kliniki ya mafunzo ya soka la wanawake katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, Sundhage alisema hana wasiwasi na soka la Tanzania kupiga hatua zaidi kwani anaona kuna idadi kubwa ya vipaji.

Sundhage alisema Tanzania imejipanga kuanzia kwa vijana wadogo ambao ndio chanzo cha mafanikio kwa jambo lolote.

“Kila kitu kinawezekana, wachezaji wanapatikana kupitia mfumo wa Grassroot na naamini kwamba siku moja Tanzania itakuwa vizuri zaidi ya ilivyo sasa,” alisema Sundhage na kuongeza.

“Nchi zilizowahi kufundisha mara nyingi zinazungumza soka la wanaume pekee, nimetumia ujuzi wangu kufanikisha maendeleo ya soka la wanawake,” alisema.

Aidha Sundhage alisema aliyoyaona kwa soka la Tanzania anaona kwamba wana mwelekeo wa kufanya vizuri zaidi.

Mwenyekiti wa soka la Wanawake Tanzania, Amina Karuma alisema kliniki hiyo itasaidia maendeleo ya soka la nchi yetu.

Karuma alisema wamelenga kufundisha makocha vijana ambao baadaye watasaidia maendeleo ya soka la wanawake ndio maana wameelekeza nguvu kwenye vyuo vya maendeleo ya Jamii ambavyo vitafanikisha kwa karibu maendeleo ya soka hilo.

Kliniki ya Karume ilishirikisha wachezaji wa timu za JKT Queens na Evergreen zote za jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku moja baada ya kutoa mafunzo kwa chuo cha Maendeleo ya Jamii Bigwa, Morogoro.

No comments:

Post a Comment

Pages