NA MWANDISH WETU
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeamuru askari Polisi aliyechukua maelezo ya mke wa Dk. Wilbroad Slaa, Josephine Mushumbusi, kumuagiza kufika mahakamani hapo Oktoba 25 kwa ajili ya kutoa ushahidi.
Jaji Sam Rumanyika alisema hayo leo wakati kesi hiyo inayomkabili Msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' ilipokuja kwaajili ya kusikilizwa ushahidi wa upande wa utetezi.
Hatua ya Jaji Rumanyika kutoa maamuzi hayo, ni baada ya Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kudai kuwa jitihada za kumpata Mushumbus zimeshindikana kwa kuwa yupo nje ya nchi na kwamba wanaomba kuyasoma na kuyatoa maelezo hayo ili mahakama iyatumie kama kielelezo cha upande wa utetezi.
Wakili wa Serikali, Faraja George alipinga maelezo hayo ya Wakili Kibatala ya kwamba anazifahamu sheria hivyo alitegemea kuwa aliyetoa maelezo polisi hapatikani, basi angeletwa aliyeandika maelezo hayo ili aweze kutoa taarifa hiyo.
" Kibatala hana mamlaka ya kutoa taarifa hii wala kusoma kwani hawezi kuvaa viatu vya watu wote badala yake atabaki kumuwakilisha mteja wake hivyo afuate taratibu zilizowekwa"alidai
Akitoa uamuzi huo, Jaji Rumanyika alisema swali la msingi ni nani atakayeitoa taarifa hiyo mahakamani kati ya wakili na aliyeandika maelezo.
"Kupatikana kwa shahidi imekuwa ngumu lakini anayepaswa kutoa maelezo hayo ni yule ambaye ameshindikana kufika mahakamani hapo na mwengine anayetakiwa kutoa maelezo hayo ni askari Polisi namba E 103 Nyangea aliyerekodi maelezo hayo, Hivyo askari huyu anatakiwa kuja kesho (leo) kutoa maelezo na hati ya wito apatiwe," alisema Jaji Rumanyika.
Katika kesi ya msingi namba 125 ya mwaka 2012, inadaiwa kuwa Aprili 7, 2012 Sinza Vatican jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua Msanii wa filamu, Steven Kanumba bila kukusudia.
No comments:
Post a Comment