Naibu Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa
Naibu Waziri wizara hiyo Mhe. Anastazia Wambura leo mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza ameahidi kushirikiana
na Watendaji wa Wizara, wadau pamoja na wananchi kwa ujumla kusimamia maadili
ya Mtanzania ili kuendelea kuwa na taifa bora.
Mhe. Shonza ameyasema
hayo alipowasili katika ofisi za Wizara leo mjini Dodoma ambapo alipokelewa na Waziri
mwenye dhamana Dkt. Harrison Mwakyembe, viongozi wa Wizara pamoja na watumishi.
“Wizara hii ni muhimu
sana kwa kuwa inajenga taswira ya taifa kupitia sekta zake ambazo ni
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo hivyo ntahakikisha tunashirikiana kwa karibu
katika kuwatumikia wananchi “alisema Naibu Waziri Shonza.
Aliongeza kwa kueleza
kuwa atahakikisha suala la maadili bora kwa jamii linazingatiwa ili kuendelea kujenga taifa
imara kwa kuzingatia mavazi yenye heshima na nyimbo zenye kujenga.
Aidha, Naibu Waziri Shonza
amesema ni wajibu wetu kama watumishi wa umma kuhakikisha tunatekeleza Ilani ya
chama tawala ambacho kiliahidi kuwatumikia watanzania ili kuhakikisha malengo
ya Serikali yanafikiwa kwa wakati.
Naye aliyekuwa Naibu
Waziri wa Wizara hiyo Anastazia Wambura amempongeza Naibu Waziri Shonza kwa
kuteuliwa kushika wadhifa huo na amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa kumuamini kuwatumikia Watanzania.
Akizungumzia utendaji
kazi, Mhe. Wambura ameufananisha utumishi wa umma na chombo cha usafiri ambapo
abiria hushuka kituo mara baada ya kufika na dereva kuendelea na safari.
“Mhe.Waziri, viongozi
wenzangu na ndugu zangu watumishi wa Wizara, mimi nimefika kituoni, Naibu
Waziri nakukabidhi kijiti endelea na safari, endelea kuwatumikia Watanzania
kama ambavyo ilani ya chama tawala inavyoeleza” alisema Mhe.Wambura
Kwa upande wake Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amemuahidi Naibu
Waziri Shonza ushirikiano wa hali na mali katika kuwahudumia wananchi kupitia
sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
No comments:
Post a Comment