Na Beatrice
Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Shirika la Majisafi
na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) limejipanga kufikisha asilimia 85 ya
upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama jijini Dar es salaam ifikapo June
mwaka 2018.
Akizungumza katika
kipindi maalumu cha TUNATEKELEZA
kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC), Afisa Mtendaji Mkuu DAWASCO
Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa takribani shilingi bilioni 114
zimepatikana kutoka benki ya dunia ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu na
zitatumika kuboresha miundombinu ya maji katika jiji la Dar es salaam.
"Kwa sasa
DAWASCO inazalisha lita milioni 510 za maji ambapo mpaka sasa Shirika limewaunganisha
wananchi wa kawaida 25,000 wanaolipa kwa awamu na kuendelea kuunganisha wateja
wapya” amesema Mhandisi Luhejema.
Aidha, Mhandisi Luhemeja
ameishukuru Serikali hasa katika kipindi hiki cha miaka miwili kuiwezesha
DAWASCO kusambaza huduma ya maji kutoka asilimia 67 hadi asilimia 75 ikiwa na
lengo la kufika asilimia 95 mwaka 2020.
“Tunataka kuhakikisha
tunaongeza uzalishaji wa maji na kwa ushirikiano tunaoupata kwa sasa
tutahakikisha tunatatua changamoto ya upatikanaji wa maji ili huduma hii muhimu
iweze kuwafikia wakazi wengi zaidi katika maeneo tunayohudumia." Alisema
Mhandisi Luhemeja.
Vilevile Mhandisi
Luhejema ameongeza kuwa DAWASCO ina visima 32 vya maji vilivyopo katika maeneo mbalimbali
ya jijini Dar es salaam na mabwawa tisa kwa ajili ya kusafisha maji ikiwa
mabwawa yenye takribani kilometa 300 yaliyopo katikati ya jiji.
Mbali na hayo,
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa DAWASCO inashirikiana na Mamlaka ya Maji safi na
maji taka Dar es salaam (DAWASA) katika kuhakikisha kuwa visima vya Kimbiji na
Mpera vinakamilika na kuanza kuzalisha maji kwa wakati.
No comments:
Post a Comment