HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 27, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kaimu Mkurugenzi wa JNIA

Jengo la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
 
 DAR ES SALAAM, OKTOBA 27, 2017
 
Uongozi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), umesema mizigo ya abiria wafanyabiashara inalazimika kufunguliwa na Maafisa wa Idara ya Forodha kutokana na Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2008 kifungu 37(1), (2) na 38, ambavyo huwaruhusu kujiridhisha kwa kufahamu kilichopo kwenye mzigo kwa kuona kwa macho kwa kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao kwa kutokuwa waaminifu hukwepa kulipa kodi.
 
Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Johannes Munanka amesema baadhi ya wafanyabiashara sasa wamebuni mbinu ya kubeba mizigo yao kwenye maboksi na mabegi makubwa yenye bidhaa mbalimbali badala ya kupitishia eneo la mizigo, hivyo hutakiwa kuyafungua wenyewe ili maafisa wakague bidhaa na kuwataka kulipia ushuru kulingana na mzigo uliopo.
 
Bw. Munanka amesema hakuna mzigo wa abiria unaofunguliwa au kumwagwa chini na aidha mfanyakazi wa JNIA, Forodha au watoa hudumu ya mizigo kwani abiria anatakiwa afungue mwenyewe mizigo yake mbele ya maafisa kwa sababu ya kiusalama na kulipia ushuru

“Natoa rai na wito kwa abiria wafanyabiashara wenye mizigo mikubwa ya bidhaa mbalimbali kutoa ushirikiano kwa maafisa wa Forodha wanapowataka kuifungua kwa ajili ya ukaguzi zaidi,” amesema Bw. Munanka.
 
Amesema mizigo ya abiria wanaowasili kutoka nje ya nchi huondolewa kwenye mkanda wa mizigo (conveybelt) na wahudumu wa ndege walizowasili nazo na kuhifadhiwa eneo la karibu na wanapomaliza taratibu zote za Uhamiaji ikiwemo ya kulipia viza huichukua mwenyewe.
 
“Hakuna mzigo au mizigo ya abiria inapotea hapa JNIA, kwani utaratibu wa mashirika ya ndege zinazowasili kutoka nje ya nchi kwa mfano Emirates wamekuwa na utaratibu mzuri wa kutoa kwenye mkanda mizigo ya abiria wao waliokwenda kushughulikia taratibu za kiuhamiaji na kuiweka sehemu moja huku wakiweka tangazo linaloonesha ni mizigo ya ndege yao na inakuwa rahisi abiria kuupata mara moja bila usumbufu, ila natoa wito mtu kama ni mgeni aulize mhudumu wa ndege aliyowasili nayo,” amesema Bw. Munanka.
 
Bw.Munanka amesema JNIA inavifaa vya ulinzi na usalama zikiwemo kamera (CCTV), ambazo zinarekodi matukio endapo kutatokea wizi na udokozi matukio yote yataonekana.
 
Amesema zinapowasili ndege zaidi ya moja kwa kutofautiana dakika chache kumekuwa na mizigo mingi kwenye mkanda, hivyo kiusalama na kuepusha msongamano na kuchanganyika kwa mizigo ya ndege moja na nyingine, wahudumu wa ndege husika wa ndani ya kiwanja wanaiondosha na kuiweka mita chache pembeni ya mkanda na kufanya abiria waione kirahisi. Hii ndilo jambo pekee mzigo unaondolewa bila mwenyewe kuwepo.
 
Hata hivyo, amesema abiria wa kimataifa na ndege za ndani (domestic) wamekuwa wakitumia milango na kumbi tofauti, lakini hulazimika kutumia mlango mmoja endapo ndege hiyo ya ndani kwa Mfano. Fastjet ikiwasili kutoka Entebbe na kuchukua abiria Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), ili taratibu za Uhamiaji zifuatwe inalazimika abiria wote wapiti mlango wa Kimataifa na kuonesha pasi za safari na wanaruhusiwa mara moja baada ya kufanyiwa ukaguzi ikiwa ametokea KIA, na wale waliotoka Entebbe watatakiwa kufuata taratibu za uhamiaji na wote wanatoka kwa kupitia mlango mkubwa na hakuna msongamano.
 
Lakini, Bw. Munanka amesema sasa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeanza mkakati wa upanuzi wa ukumbi wa kuwasili wa abiria wa kimataifa, ambapo panakuwa na msongamano unaosababishwa na uombaji viza mara wanapowasili, ambapo sasa yataongezwa madirisha zaidi ya huduma hiyo inayotolewa na Idara ya Uhamiaji pamoja na benki ya NMB.
 
Imetolewa na Uongozi wa JNIA
 
Kaimu Mkurugenzi JNIA
 
26/10/2017

No comments:

Post a Comment

Pages