HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 08, 2017

NYUMBA ZILIZOJENGWA BILA VIBALI KUVUNJWA ZANZIBAR


Balozi Seif akiuagiza Uongozi wa Wilaya ya Magharibi A kusimamia sheria na taratibu dhidi ya watu wanaoamua kujenga bila ya kuzingatia Sheria zilizowekwa.
 Kasi ya maji ya mvua yanayoonekana yakititirika katika Mto wa Bububu kutokana na baadhi ya Watu wengi kutozingatia njia za maji hayo kutokana na ujenzi holela.

 WILAYA YA MAGHARIBI 'A', ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba katika utaratibu wa kunusuru Maafa hasa kwenye maeneo hatarishi Serikali Kuu italazimika kuvunja majengo yote yaliyojengwa bila ya kuzingatia sheria za ujenzi zilizowekwa.

Alisema baadhi ya nyumba zisizozingatia Mfumo wa Mipango Miji, Mamlaka zinazosimamia Ujenzi zitalazimika kuchukuwa hatua dhidi ya watu wote waliojenga bila ya kupata vibali kutoka Mamlaka hizo.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziafa fupi ya kuzipa pole familia za Watu waliofiwa na jama zao pamoja na kukagua maeneo yaliyoathariki kutokana na maafa ya mafuriko ya Mvua za Vuli katika Shehia ya Bububu Kijichi Wilaya ya Magharibi “A”.

Alisema wakati umefika kwa Jamii kulazimika kufuata Sheria za Nchi na kuacha tabia ya muhali ambayo kwa kiasi kikubwa tayari imeshaathiri Jamii kwa kiasi kikubwa katika masuala mbali mbali likiwemo lile sugu lililoshamiri hivi sasa la ushalilishaji wa Kijinsia.

Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba Wananchi wasipozingatia taratibu za Nchi hata zile za Dini pamoja na Kimila Jamii itaelekea mahali pabaya pa maangamizi na ni vyema hali hiyo ikapaswa kutafutiwa dawa ya haraka.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitoa Mkono wa pole kwa Familia ya Bwana Hussein Khamis Hamad aliyefiwa na Mama yake Mzazi Marehemu Bibi Salma Khamis na Bwana Rajab Moh’d aliyeondokewa na Mtoto wake.

Balozi Seif alizitaka Familia hizo kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba wa wapendwa wao na wanapaswa kukubali kuwa matukio hayo ni kudra za Mwenyezi Muungu.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A” Kepteni Khatib Khamis alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba sababu kubwa iliyopelekea maeneo ya Bubu Kijichi kukumbwa na mafuriko ya maji kunatokana na baadhi ya Watu kutozingatia utaratibu wa Ujenzi.

Kepteni Khatib alisema baadhi ya Watu wameshindwa kufuata Sheria za Ujenzi licha ya kwamba Viwanja walivyopewa vilipata baraka ya upimwaji halali na hatimae kuvuruga Mipango hiyo.

Alisema zipo nyumba zilizojengwa katika vianzio vya Maji na nyengine zimetiwa kuta ndani ya mitaro ya mito ya maji kitendo ambacho kimezalisha maafa yanayoweza kuepukwa mapema.

Alihafamisha kwamba kasi ya maporomoko ya maji itaongezeka na maafa yataendelea kushuhudiwa iwapo wajenzi holela katika maeneo yao hawatadhibitiwa mapema.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

7/11/2017.

No comments:

Post a Comment

Pages