WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia
sh. bilioni 11.9 kufanya ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na
mabweni katika vyuo 10 vya ualimu nchini.
Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Morogoro, Mpwapwa, Butimba, Kasulu, Songea,
Tukuyu, Marangu, Kleruu, Korogwe na Tabora. “Ukarabati huu umewezesha wanachuo 5,920
waliokuwa wanasoma Stashahada maalum ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA katika Chuo
Kikuu cha Dodoma kuhamishiwa katika vyuo hivyo,” ameongeza.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Novemba 17,
2017) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya
kuahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Januari 30,
mwakani.
Amesema ili kuongeza fursa za wanafunzi kusomea
ualimu, Serikali imepanga kujenga na kukarabati vyuo vya ualimu vya Kitangali,
Ndala, Mpuguso na Shinyanga kwa thamani ya sh. bilioni 36.47.
Amesema mradi huo ambao utatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2016/2017
- 2018/2019, unalenga kuongeza fursa kwa wanafunzi wenye sifa kupata nafasi ya
kujiunga na elimu ya ualimu.
“Ujenzi na ukarabati huu utasaidia kuongeza udahili katika vyuo vya
ualimu vya Serikali kutoka wanachuo 20,535 katika mwaka 2017 hadi kufikia wanachuo
23,835 katika mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la wanachuo 3,300,” amesema.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza maandalizi ya
awamu ya pili ya ukarabati wa vyuo saba vya ualimu vya Serikali. Amevitaja vyuo
hivyo kuwa ni Tandala, Nachingwea, Tarime, Kinampanda, Mandaka, Patandi na
Ilonga.
Amesema vyuo vya ualimu vya Murutunguru, Kabanga na Mhonda vitalazimika
kujengwa upya baada ya wahandisi kubaini kuwa vyuo hivyo havifai kukarabatiwa
kutokana na uchakavu mkubwa wa majengo yake.
Wakati huo
huo, Waziri Mkuu amesema ili kukabiliana na upungufu wa
wahadhiri kwenye vyuo vya elimu ya juu, katika mwaka 2017/18, Serikali imepanga
kusomesha wahadhiri 100 katika ngazi za shahada za umahiri na uzamivu.
Waziri Mkuu amesema kati ya mwaka 2016/17 na 2017/18, Serikali imeratibu
upatikanaji wa wanafunzi wa Kitanzania wanaofadhiliwa kusoma nchi za nje ambapo
China wapo wanafunzi 86, Uingereza (17), Misri (4), Korea (3), Urusi (13) na
Thailand (2) huku baadhi ya wanufaika wakiwa ni wahadhiri wa vyuo vikuu na
taasisi nyingine za elimu ya juu nchini.
Vilevile, kupitia kuimarika kwa mahusiano yetu ya kidiplomasia, Waziri
Mkuu amesema, Septemba, mwaka huu, Serikali ilitia saini makubaliano na nchi ya
Hungary ambapo itakuwa inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 30 kwa kipindi
cha miaka mitatu kuanza mwaka 2018/2019.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA,
NOVEMBA 17, 2017
No comments:
Post a Comment